Katika hali inayoonesha kuwa wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro
wamepuuza ushawishi wa baadhi ya watu wanaotaka wasiondoke katika eneo hilo,
leo tarehe 3 machi, 2024 jumla ya kaya 76 zenye watu 451 na mifugo 1,259 wameamua
kuondoka kwa hiyari ndani ya hifadhi hifadhi kuelekea katika Kijiji cha Msomera
wilayani Handeni Mkoani Tanga na kijiji cha Makao wilayani Meatu mkoani Simiyu.
Katika hafla ya kuwaaga wananchi hao iliyofanyika makao makuu
ya zamani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro baadhi ya wananchi wamesema kuwa
wameamua kuondoka ndani ya hifadhi kutokana na kufanya mawasiliano na wenzao
waliokwishahamia katika Kijiji cha Msomera na kupata taarifa kuwa maisha katika
Kijiji hicho ni bora kulinganisha na kuishi hifadhini.
“Hatuondoki kwa kukurupuka,tunafanya mawasiliano na wenzetu
ambao tayari wameshakwenda Msomera na wakati mwingine tumekuwa tukifika katika
Kijiji hicho kufanya uchunguzi, binafsi kabla ya maamuzi haya nilikwenda
Msomera kufanya uchunguzi wangu na
kushuhudia maendeleo makubwa katika kijiji hicho, ndiyo maana niliporudi
Ngorongoro niliishawishi familia yangu na leo tumeamua kuondoka,” alisema Bwana
Mathayo Laizer mmoja wa wakazi walioamua kuhama kwa hiyari.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw.
Richard Kiiza amewaambia wananchi hao kuwa serikali imejipanga vizuri
kuhakikisha wananchi hao wanapata haki zao zote za msingi ikiwa ni pamoja na
huko wanakokwenda kuwepo kwa miundo mbinu mizuri itakayowawezesha kuboresha
maisha yao ya kila siku.
Kamishna Kiiza amesema kila mwananchi ambaye yupo tayari
kuhama atasafirishwa kwa wakati na kupata stahiki zake zote bila urasimu huku
akisisitiza kuwa zoezi la uandikishaji wa wananchi wanaotaka kuhama kwa hiyari
linaendelea kwa kasi katika maeneo mbalimbali ya Tarafa ya Ngorongoro.
Katika taarifa yake Kaimu Meneja Mradi wa zoezi hilo Afisa
Uhifadhi Mkuu Flora Assey amesema zoezi la kuhamasisha na kuandikisha wananachi
kuhama kwa hiyari kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro linaendelea kwa kasi
kutokana na wananchi kupata uelewa mpana wa jinsi wanavyoweza kupata fursa za
kujiendeleza kiuchumi katika maeneo wanayoelekea.
Mwakilishi kutoka wizara ya Maliasili na Utalii Bw. John
Mapepele aliwapongeza wananchi hao kutokana na kuamua kuondoka ndani ya hifadhi
na kusisitiza kuwa wizara itaendelea kusimamia zoezi hilo kwa karibu ili
kuhakikisha kila mtu anayetaka kuondoka anapewa fursa hiyo na misingi ya
sheria, taratibu na haki za binadamu itazingatiwa.
Serikali inaendelea na zoezi la kuhamisha watu kutoka ndani
ya hifadhi ya Ngorongoro lengo likiwa ni kuboresha maisha ya wananchi hao nje
ya hifadhi hasa ikizingatiwa kwamba katika eneo hilo wananchi hao wamekuwa
wakikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo uwepo wa fursa chache za kujiendeleza kiuchumi na
kijamii.
0 Maoni