Inakadiriwa kuwa watu milioni 850 duniani wanasumbuliwa na
magonjwa sugu ya figo na kati yao watu milioni 3.1 hufariki dunia kila mwaka na
kuufanya ugonjwa huo kushika nafasi ya nane ulimwenguni kwa kusababisha vifo.
Hayo yamesemwa leo na
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo kutoka Hospitali ya Muhimbili, Dkt. Jonathan
Mngumi wakati akitoa elimu kuhusu umuhimu wa kulinda na kutunza figo dhidi ya
magonjwa ikiwa ni siku ya maadhimisho ya figo Duniani ambayo huadhimishwa mwezi
Machi kila mwaka.
Ameeleza kuwa watu wengi wenye magonjwa ya figo wanakadiriwa
kuishi katika nchi zinazoendelea hususani kusini mwa Jangwa la Sahara na idadi
hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka na kwa sasa inakadiriwa kuwa wastani wa
asilimia 7 mpaka 25 ya wakazi wa Afrika wana matatizo ya figo ambapo kiasi hiki
ni mara tatu zaidi ya nchi zilizoendelea, amesema Dkt. Mngumi.
“Idadi ya wagonjwa
wanaopatiwa huduma ya kusafisha damu imefikia 3,500 nchini kote ambapo kwa
Muhimbili kila siku inahudumia wagonjwa 120 hadi 130,” amesema Dkt. Mngumi.
Dkt. Mngumi ameitaka jamii kubadili mtindo wa maisha kuacha
matumizi makubwa ya sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi na kufanya mazoezi
mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa mbalimbali kama vile kisukari na
shinikizo la damu ambayo yameonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa magonjwa ya
figo.
Kauli mbiu mwaka ya huu inasema “Afya ya figo kwa wote,
kuendeleza usawa katika ufikiaji wa huduma na matumizi bora ya dawa”
0 Maoni