WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria
kuhakikisha usalama wa nchi na mipaka yake dhidi ya majanga mbalimbali
unaendelea kuimarishwa ili kujiandaa na kuwa na utayari wa kukabiliana na
majanga, maafa na dharura yoyote.
Ametoa kauli hiyo jana Machi 14, 2024, wakati wa ufungaji wa
mafuzo ya zoezi la utayari dhidi ya
dharura za kikemikali na kimionzi Tanzania, katika viwanja vya Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji, Bandarini jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa moja ya jitihada hizo ni pamoja na kukamilisha
maandalizi ya nyaraka mbili muhimu za Mpango wa Kitaifa wa Maafa ya Kikemikali,
Kibaiolojia, Kiradiolojia na Kinyukilia. (CBRN National Action Plan) na Mpango
wa Kuitikia wakati wa Dharura za Kinyuklia na Kiradiolojia (Radiological and
Nuclear Response Plan) ambazo alizizindua katika hafla hiyo.
“Kupitia nyaraka hizi, mmeweka mikakati ya pamoja ya kitaifa
ya namna ya kukabiliana na kujikinga na majanga yatokanayo dharura za
kikemikali, kibaiolojia, kiradiolojia na kinyuklia. Nimefurahi sana kusikia
nyaraka hizo zimezingatia masuala muhimu ya kisera, uzoefu wa kukabiliana na
majanga kitaifa na kimataifa pamoja na matakwa ya kisheria na itifaki za
kimataifa.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka wizara zote na taasisi
zinazohusika na kutekeleza mipango hiyo kuitumia kikamilifu na zitoe
ushirikiano kwa wote wanaohitaji kutekeleza miongozo hiyo “Miongozo hii isiwe
ni nyaraka za makabatini tu bali iwe miongozo ya utekelezaji wa hatua thabiti
za kuhakikisha tunajenga nchi imara na salama. ”
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Prof. Profesa Adolf Mkenda amesema mafuzo ya zoezi la utayari dhidi ya dharura za kikemikali na
kimionzi yalilenga kuwapa washiriki maarifa na ujuzi wa kukabiliana na vitisho
vya kikemikali, kiradiolojia, kinyuklia na kusaidia juhudi kujiandaa na
kukabiliana na majanga hayo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ameongeza kuwa nyaraka zilizozinduliwa na Mhe. Majaliwa
zitatumika kuwa nyaraka za kitaifa na miongozo inayochukua mitizamo na mahitaji
ya taasisi na wizara mbalimbali za Serikali na wadau wengine waliopewa majukumu
katika nyanda za kemikali, kibaolojia, kiradiolojia na nyuklia “Lengo kuu la
mipango hii ni kuweka mikakati ya pamoja kama Taifa ya namna ya kukabiliana na
kujikinga na majanga hayo. ”
Kwa Upande wake, Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice
Mafumiko amesema kuwa mazoezi ya utayari
dhidi ya dharura za kikemikali na kimionzi yataendelea kufanyika mara kwa mara
kwa lengo la kujenga utayari wa timu ya Taifa ya kujiandaa kukabiliana na
dharura za kitaifa.
0 Maoni