Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa
Serikali Bw. Mobhare Matinyi amesema Sekta ya Utalii ndiyo sekta inayoongoza
hivi sasa kwa kuiletea nchi fedha za kigeni.
Akiongea leo Dar es Salaam na Wahariri na Waandishi wa Habari
wakati akielezea mafanikio ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bw. Matinyi amesema mapato ya utalii sasa yamefikia dola
za Marekani bilioni 3.37 (zaidi ya shilingi trilioni 8).
Kimsingi sekta hii imemrejeshea shukurani Mhe. Rais Samia kwa
juhudi zake binafsi za kutoka ofisini na kwenda kushiriki katika utengenezaji
wa filamu ya “Tanzania: The Royal Tour”, amesema Bw. Matinyi.
Amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu idadi ya watalii
nchini imeongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 walioipatia nchi mapato dola za
Marekani bilioni 1.31 hadi watalii 1,808,205 mwaka 2023 walioingiza dola
bilioni 3.37.
Ameeleza kwamba kwa kuongeza idadi ya watalii wengi baada ya
mlipuko wa UVIKO-19 Tanzania sasa inashika nafasi ya pili barani Afrika baada
ya Ethiopia; na kwa kuongeza mapato makubwa inashika nafasi ya tatu baada ya
Moroko na Morisi (Mauritius).
“Tanzania imeendelea kutambuliwa kimataifa na kupata tuzo
mbalimbali. Tuzo hizo ni Hifadhi ya Taifa Serengeti kuwa hifadhi bora barani
Afrika kwa miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi 2023,” amesema Bw.
Matinyi.
Pia, amesema Tanzania kuwa nchi ya saba miongoni mwa nchi 18
duniani zilizo bora kutembelewa kiutalii kwa mwaka 2022, ambapo Hifadhi ya Taifa
Serengeti kuorodheshwa kama eneo maridhawa la kutembelewa kwa mwaka 2023 na
Hifadhi ya Taifa Serengeti kushika nafasi ya tatu ya vivutio bora vya asili
duniani kwa mwaka 2023.
Aidha, Bw. Matinyi amesema Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya
Ngorongoro imeshinda tuzo mbili za Best of the Best Travelers’ Choice na
Africa’s Leading Tourist Destination kwa mwaka 2023. Hizi ni baadhi ya tuzo
ambazo Tanzania imezipata kimataifa; si zote.
0 Maoni