Rekodi ya idadi ya watalii wa kigeni waliotembelea Hifadhi ya
Urithi wa Dunia na Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara iliyo chini ya
usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA Machi 4, 2024
imevunjwa baada ya kupokea meli ya nane kutia nanga Hifadhini humo ikiwa na
watalii 125 kutoka Mataifa mbalimbali na hivyo kufikisha jumla ya watalii 925
waliotembelea hifadhi hiyo katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Februari 03,
2024.
Kwa mujibu wa takwimu za idadi ya watalii wa kigeni waliotembelea
hifadhi hiyo katika kipindi cha hivi karibuni mwaka 2024 umetajwa kuwa ni mwaka
wenye mafanikio makubwa kwa TAWA kupata safari nyingi za meli za watalii
kupitia Hifadhi hiyo yenye urithi wa kihistoria na kiutamaduni, ukongwe wa
magofu ya kale yaliyojengwa kwa ustadi mkubwa kiasi cha kustaajabisha na
kuvutia watalii mbalimbali wanaotembelea hifadhi hiyo
Imeelezwa kuwa takwimu za miaka mitatu kuanzia mwaka 2022,
idadi ya meli zilizotia nanga hifadhini humo zilikuwa mbili (2) zikiwa na zaidi
ya watalii 200, ambapo mwaka 2023 meli 3 ziliwasili katika hifadhi husika
zikiwa na zaidi ya watalii 300 na mwaka huu wa 2024 meli zipatazo nane zikiwa
na zaidi ya watalii 900 zimetia nanga hifadhini humo.
Ongezeko hilo la watalii katika Hifadhi hiyo ni ishara kuwa
utalii wa malikale unazidi kuchechemka nchini ukichagizwa na jitihada za dhati
zilizofanywa na Mhe. Dr. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania katika kuitangaza Nchi yetu na vivutio vyake kupitia filamu maarufu ya
Tanzania The Royal Tour iliyoleta matokeo makubwa kwa muda mfupi.
Pia nguvu kubwa ya kuwekeza katika kuboresha miundombinu
wezeshi ya utalii iliyofanywa na Serikali kupitia TAWA ambayo imechangia kwa
kiasi kikubwa kuvutia watalii wengi kutembelea hifadhi hiyo lakini bila kusahau
mchango mkubwa wa Sekta binafsi katika kutangaza vivutio vya utalii wa Nchi
yetu.
Hii ni dalili tosha kuwa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 na malengo ya Serikali ya kufikisha idadi ya
watalii Million 5 na mapato ya takribani dola billioni 6 ifikapo mwaka 2025
yanakwenda kufikiwa kwa kishindo na TAWA ikiwa ni miongoni mwa taasisi
zinazoshiriki katika kuchangia kufikia malengo hayo.
Na. Beatus Maganja- Kilwa
0 Maoni