MITATU YA SAMIA: Wageni 6,931 wafuata matibabu nchini 2023

 

Uwekezaji katika Sekta ya Afya uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka mitatu, umechangia kuboresha huduma za kibingwa na kibobezi nchini na kuwavutia wagonjwa kutoka nje ya nchi kuja kutibiwa nchini Tanzania.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Mobhare Matinyi amesema kwa mwaka 2023, idadi ya wagonjwa kutoka nje ya nchi waliokuja kutibiwa nchini ilikuwa 6,931 ikilinganishwa na wagonjwa 75 mwaka 2021.

“Wagonjwa hawa wanatoka katika nchi za Komoro, Malawi, Burundi, Zambia, DRC, Uganda, Zimbabwe na Kenya,” alisema Bw. Matinyi katika mkutano wake huo leo aliouitisha kuelezea mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Samia.

Ameeleza kuwa wagonjwa hao walihudumiwa katika hospitali sita ambazo ni Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Taasisi ya Mifupa (MOI) pamoja na hospitali binafsi za Aga Khan na Saifee.

Amesema Serikali ili wekezaji katika sekta ya afya kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa ulifikia jumla ya shilingi bilioni 916.6 katika miaka mitatu ambapo zililenga kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya ya msingi.

Akielezea matumizi ya fedha hizo Bw. Matinyi amesema kwamba zilitumika katika ujenzi na uendelezaji wa hospitali mpya za halmashauri 127 ambapo kati ya hizo hospitali 25 zimeanza kujengwa kipindi cha awamu ya sita.

Pia, fedha hizo zilitumia katika ukarabati wa hospitali kongwe 50 za halmashauri, ujenzi wa vituo vya afya 367, ukamilishaji wa majengo ya zahanati 980, ujenzi wa majengo 83 ya kutolea huduma za dharura (EMD) na majengo 28 ya huduma kwa wagonjwa mahututi (ICU).

Maeneo mengine ni ujenzi wa kituo cha kutibu magonjwa ya milipuko, ujenzi wa mitambo 21 ya kuzalisha oksijeni kwa ajili ya wagonjwa mahututi na wa dhararua, ujenzi wa nyumba za watumishi 270, ununuzi wa vifaa vya tiba zikiwemo mashine za mionzi ya X za kidigitali, Kuajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya 17,137 pamoja na ununuzi wa magari 528 yakiwemo ya kubebea wagonjwa 316.

Bw. Matinyi ameeleza kwamba kwa ujumla wake, kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Afya, Serikali imenunua jumla ya magari ya kubebea wagonjwa 727 ambapo hadi sasa 327 yameshapokelewa na kusambazwa nchini.

Kuhusu bajeti ya manunuzi ya dawa Bw. Matinyi amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza fedha za ruzuku ya kununulia dawa kutoka Bohari Kuu (MSD) ambapo kwa mwaka 2021/22 ilikuwa shilingi bilioni 29.3 lakini kufikia mwaka 2022/23 zimefikia shilingi bilioni 120.8.

“Kuanzia Julai 2023 hadi Februari 2024 tayari Serikali imeshatoa shilingi bilioni 74.5 na Serikali inaendelea kutoa zaidi,” amesema Bw. Matinyi. 

Pamoja na mambo mengine, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya kutolea huduma za afya ambapo vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka kutoka vituo 8,549 mwaka 2021 hadi kufikia vituo 9,610 Machi 2024 - ongezeko la vituo 1,061 (12.4%).

Mgawanyo hadi kufikia Machi 2024 ni Zahanati 7,999, Vituo vya afya 1,170, Hospitali za halmashauri 172, Hospitali zenye hadhi ya wilaya 181, Hospitali za rufaa za mikoa 28, Hospitali zenye hadhi ya mkoa 36, Hospitali za rufaa za kanda 5, Hospitali zenye hadhi ya kanda 12, Hospitali maalum 6 na Hospitali ya Taifa moja.

Chapisha Maoni

0 Maoni