Utekelezaji wa miradi ya barabara katika Halmashauri ya
Manispaa ya Singida upo hali nzuri kwa asilimia 75 ya miradi yote
inayotekelezwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi Ibrahimu Kibasa
amesema Manispaa hiyo ina jumla ya mtandao wa barabara wenye urefu wa Km. 523.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea miradi miwili
inayotekelezwa ndani ya Manispaa hiyo, amesema Singida imetengewa bajeti ya
barabara yenye jumla ya Shilingi bilioni 2.7.
“Tumetembelea miradi ya miradi miwili ya barabara ambayo
imekuwa ikiendelea kutekelezwa na wakandarasi wetu eneo la hapa mjini,” amesema
na kuongeza,
“Miradi hiyo ni ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami eneo
la Mnung’una mkataba unagharimu Shilingi Milioni 575,” amesema.
Mhandisi Kibasa amesema ujenzi huo unasimamiwa na mkandarasi
JAM contractor unatekelezwa kwa muda wa miezi minane mpaka sasa amefikia 96% ya
utekelezaji.
“Ulitakiwa kukamilika 17 Mei, 2024, lakini utamalizika kabla
ya muda, amefanya kazi yake kama vile inavyotakiwa.
Amesema mkataba wa pili wa ujenzi wa barabara katika kiwango
cha lami eneo la Mwenge-Mungumaji unatekelezwa na Mkandarasi Jp Contractor.
“Umegharimu Shilingi Milioni 611 na ulikuwa ukitekelezwa kwa
muda wa miezi sita, umefikia 90% ya utekelezaji, tunatarajia hivi karibuni
atamalizia kazi zake na atakabidhi” amebainisha.
Amesema ujenzi wa barabara hizo una tija kwa jamii kwani
wamejenga katika maeneo wanakoishi wananchi ambako hapo kabla walikuwa wakipata
changamoto lukuki.
“Tuna uhakika tumeboresha maisha ya wananchi, tutakuwa
tumeongeza shughuli za ki-biashara na tumepandisha hadhi ya maeneo yao.
“Kwa hiyo hata wale wenye maduka na vitu vyao vilikuwa
vikiharibiwa na vumbi kwa sasa thamani ya bidhaa zao zitabaki katika hali
halisi.
Ameongeza “Wakala tutaendelea kuboresha barabara za Manispaa
na halmashauri nyinginezo kwa kuhakikisha zinakuwa katika ubora.
“Kwa kiwango cha lami, changarawe na kujenga madaraja katika
kaeneo mbalimbali yaliyo na changamoto.
“Tunashukuru Singida tuna mawe mengi katika mkoa wetu,
tunahakikisha tunatumia malighafi zilizopo kwenye eneo husika ili kupunguza
gharama za ujenzi,” amesema.
Amesema kwa kutumia rasilimali za ndani ya maeneo husika imekuwa manufaa pia kwa kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.
“Kwa hiyo tumekuwa tukijenga madaraja ya mawe katika maeneo
mengi katika wilaya nyingi, hata hapa Singida.”
“Singida mjini badala ya kutumia zege peke yake tumekuwa
tunatumia mawe, kwa kutumia rasilimali zilizopo na wananchi wanapata Kipato.”
“Wanapeleka watoto shule na maisha mengine yanaendelea,
tunaongeza pato la mtu mmoja mmoja.”
Mhandisi Kibasa amewasihi wananchi kuendelea kutunza
miundombinu kwa ushirikiano wa karibu na viongozi wao katika maeneo yao ili
idumu.
“Wawe walinzi wa miundombinu kwa sababu tunaamini zile
barabara ambazo zimetengenezwa zimetokana na kodi za wananchi”.
“Unapobomoa unaifanya Serikali irudi kutengeneza tena wakati
ingeenda eneo jingine au fedha zingeenda kutumika kwenye huduma zingine,”
ametoa rai.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa eneo
hilo, wamekuwa na mtizamo chanya kuhusu ujenzi huo wa miundombinu.
Wameipongeza TARURA na Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais
Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa miundombinu imara.
Mkazi wa eneo la Mwenge Bw. Leonard Kwayu amesema amekuwa
hapa tangu mwaka 1998, walikumbana na changamoto nyingi barabarani.
“Walipokuja kuanza kuitengeneza sasa ipo vizuri, mitaro ipo
vizuri, changamoto ilikuwa kwa sababu ya udongo. Ilikuwa inachimbika sana
ilikuwa na mashimo mengi, sasa hivi serikali inatujali.., tumeona imetujali,”
amesema.
Naye Bi. Devotha Charles ameongeza kuletewa lami mtaani kwao,
barabara ilikuwa mbaya ilikuwa na mawe sasa imekuwa neema.
“Hata wafanyabiashara tunaonekana vizuri, tunashukuru uongozi
wa Mama Samia umetuokoa”.
“Itatusaidia kwa biashara zetu hata wagonjwa watasafiri
vizuri, barabara imekuwa vizuri,” amesema na kuipongeza TARURA.
“Wamekuwa wepesi kuona hizi barabara za mtaabni nasi tumepata
lami, waangalie na kwengine ambako hakuna wawawekee lami,” ameomba.

0 Maoni