Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa ameielekeza Wakala wa Mabasi yaendayo
haraka (DART) kufikia mwezi Oktoba 2024 iwe imempata mwekezaji binafsi ambaye
ni mtoa huduma wa mabasi hayo ili kuleta ufanisi.
Mchengerwa ametoa maelekezo hayo wakati akiwasilisha Randama
ya Bajeti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI Fungu namba 56 na Fungu namba 2 la Tume ya
Utumishi wa Walimu mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa katika ukumbi wa Anne Makinda uliopo bungeni jijini Dodoma.
“Nilishawambia watu wa ‘DART’ wakati wanakuja kunipitisha
kwenye mfumo tunaokwenda nao ikifika mwezi Oktoba wakishindwa kuhakikisha
wanampata mwekezaji atayekwenda kuhudumia njia hii wa Private sekta na
kushindwa kuhakikisha mabasi yamepatikana waniletee barua za kujiuzulu na
tumeshakubaliana na hakuna mjadala watu wanataka huduma,” amesema Mchengerwa.
Akisisitiza hilo Mchengerwa amesema kuwepo kwa mwekezaji
binafisi katika mradi huo utaendeshwa kwa ufanisi kutokana na kulipa kodi kwa
serikali na wakati huohuo atawajibika endapo atatoa huduma isiyostahili.
“Atahakikisha anatoa huduma nzuri ili watu waweze kuhudumiwa
na kama tukileta mabasi ya kutosha watu wa Dar es Salaam watapaki mabasi yao
watatumia mwendokasi na tutakwenda kuokoa zaidi ya sh.bilioni 300 ambayo
tungeitumia kununua mabasi,” amesema Mohammed Mchengerwa.
Hata hivyo Mchengerwa amesema ifikapo mwezi Septemba hadi
Oktoba serikali itakuwa imepata mabasi ya kutosha ya kuendesha njia zote kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi ili watanzania wa Dar es
Salaam waweze kuhudumiwa vizuri kabla ya kuanza kupeleka huduma ya mwendokasi
katika majiji mengine.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Denis Londo
amepongeza uamuzi huo na kusema kuwa maamuzi hayo yaacha alama nzuri wa Waziri
aliyepo kutokana na ubunifu huo.
CHANZO: OR-TAMISEMI

0 Maoni