WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Elimu,
Sayansi, na Teknolojia, iandae mpango maalum wa ufadhili wa wataalam wa lugha
ya Kiswahili kwenye ngazi ya shahada ya
uzamivu ili kukidhi mahitaji sambamba na
kuimarisha mafunzo ya lugha kwa ajili ya kuzalisha wataalam na wakalimani wa
kiswahili wenye viwango vya kimataifa.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo jana wakati alipomwakilisha
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kongamano la Nne la
Idhaa za Kiswahili Duniani linalofanyika katika Hoteli ya Eden Highlands jijini
Mbeya.
Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua kadhaa ili
kukibidhaisha Kiswahili na moja ya hatua hizo ni kuandaa Mkakati wa Taifa wa
kubidhaisha Kiswahili ambao una lengo la kuifanya lugha hiyo kuwa bidhaa kwa kutoa fursa za kujikwamua kiuchumi kwa
rasilimaliwatu wanaojihusisha nayo pamoja na watoa huduma za kiswahili.
Amesema Serikali imeendelea kuhakikisha balozi zetu zinakuwa
kitovu cha kueneza Kiswahili katika nchi za ughaibuni, ili kufanikisha azma
hiyo, Serikali imeratibu ufunguzi wa vituo vipya vya kufundisha Kiswahili
katika balozi mbalimbali za Tanzania ughaibuni.
Miongoni mwa nchi hizo ni Uholanzi, Falme za Kiarabu za Kiarabu na
Dubai, Ujerumani, Italia, Zimbabwe, Nigeria, Comoro, Ufaransa, Korea na Uturuki.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameelekeza kuwa nyaraka za
mawasiliano za wizara, idara na taasisi zake ziandikwe kwa Kiswahili sanifu,
vilevile, mikutano, warsha, dhifa, semina na mijadala ya umma iendeshwe kwa
lugha ya Kiswahili.
“Sheria, kanuni, miongozo na mipango mkakati ambayo bado
haijatafsiriwa kwa Kiswahili, itafsiriwe kwa kushirikiana na Mabaraza ya
Kiswahili (BAKITA na BAKIZA) na watalaamu wengine wa Kiswahili,”alieleza.
Pia ameielekeza BAKITA na BAKIZA waandae na kutekeleza mpango
wa mafunzo kwa makundi mbalimbali kama vile wahariri, wafasiri, wakalimani,
waandishi wa vitabu, walimu, makatibu muhtasi, washereheshaji na makundi
mengine mengi yanayotumia na kukieneza Kiswahili.
“…Shirika la Viwango Tanzania, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba
shirikianeni na BAKITA, BAKIZA pamoja na wataalamu wengine wa Kiswahili
kutafsiri kwa Kiswahili maelekezo ya bidhaa na huduma zinazotolewa na wadau
mbalimbali.”
Akizungumzia kuhusu lengo la kongamano hilo pamoja na mambo
mengine amesema linalenga kujadiliana kuhusu maudhui ya utangazaji kwa kutumia
lugha ya kiswahili na kutambua jitihada za vyombo vya habari katika kukifanya
kiswahili kuwa bidhaa.
“Kiswahili ni
utambulisho wa taifa letu na wote tunatambua mchango mkubwa wa Kiswahili katika
uhuru wa Tanganyika, Mapinduzi ya Zanzibar na harakati za ukombozi katika bara
letu la Afrika.”
Waziri Mkuu amesema kaulimbiu ya kongamano hilo inasema
“Tasnia ya Habari na Fursa za Ubidhaishaji wa Kiswahili Duniani”, ambayo
kimsingi inaweka msisitizo kuhusu nafasi ya tasnia ya habari katika kukinadi na
kukieneza kiswahili duniani. “Kwa upande mwingine, inaweka msisitizo katika
nafasi kubwa waliyonayo wanahabari kwa maendeleo ya lugha ya Kiswahili,” alisema.
Amesema kaulimbiu hiyo ni utekelezaji wa vitendo wa Ilani ya
uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/2025, Mpango wa Maendeleo wa
Miaka Mitano Awamu ya Tatu, Dira ya Maendeleo ya Taifa Mwaka 2025, Dira ya
Maendeleo ya Zanzibar Mwaka 2050 pamoja na Mpango wa Maendeleo ya Zanzibar
Mwaka 2021-2026.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan (wakati akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania)
kwenye ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili yaliyofanyika Jijini
Dodoma, mwezi Januari, 2021 alielekeza
Wizara zinazohusika na utamaduni nchini, zibaini maeneo ambayo bado Kiswahili
hakitumiki ipasavyo ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.
Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais, alitoa maelekezo kwa
mabaraza ya Kiswahili yaandae mikakati mahususi ya kukikuza na kukiendeleza
Kiswahili ili Serikali iyawezeshe kwa kuyapatia wataalamu na itenge fedha
katika bajeti kwa ajili ya miradi ya Kiswahili ya mabaraza haya.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Tabia Maulid amesema kwa
kushirikiana na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania Bara, Dkt.
Damas Ndumbaro watahakikisha lugha ya kiswahili inaendelea kukua kimataifa na
kuwa bidhaa muhimu katika kukuza uchumi na kuvutia utalii nchini.
Naye, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Ndumbaro
ametumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
maboresho makubwa aliyoyafanya katika wizara yao katika kipindi cha miaka
mitatu tangu Serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani.
“…Katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Mheshimiwa
Rais Dkt. Samia ametuwezesha kufungua vituo 44 vya kufundisha kiswahili na
tumeona faida yake. Vyombo vya habari 44 vinatangaza kwa kiswahili duniani na
hivyo kukiwezesha kiswahili kuzidi kukua na kupendwa duniani na kuongeza fursa
za ajira kwa wahariri, walimu na wakalimani.”
Akizungumzia kuhusu kongamano hilo, Dkt. Ndumbaro amesema
lugha ya kiswahili kwa sasa imekuwa bidhaa inayouzika kwa kasi kubwa duniani na
Tanzania imeendelea kukuza lugha hiyo kupitia utamaduni, sanaa na michezo
kupitia nyimbo na shughuli mbalimbali za kimichezo na utamaduni.
Awali, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania
(BAKITA), Consolata Mushi alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa jitihada
za kukibidhaisha Kiswahili na kuziagiza balozi za Tanzania katika Mataifa
mbalimbali kufungua madarasa ya kufundisha lugha hiyo ambapo hadi sasa vituo 16
vimefunguliwa nje ya nchi na 28 vimefunguliwa nchini.
Mapema, Waziri Mkuu alikabidhi tuzo ya heshima kwa aliyekuwa
Rais wa awamu ya Pili, Hayati Ali Hassan Mwinyi ambaye alitoa mchango mkubwa
katika kukuza kiswahili kwa kuhamasisha matumizi ya kiswahili sanifu, kukosoa
na kuelekeza matumizi sahihi ya maneno ya kiswahili. Pia alikuwa mwenyekiti wa
BAKITA (1968-1978).
Tuzo hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na
Michezo kupitia BAKITA kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na
Teknolojia ya Habari kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na
kupokelewa na mtoto wa marehemu Abdulla Ali Mwinyi.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni