WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Uchukuzi
kusimamia ipasavyo Shirika la Ndege Tanzania ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa
uliofanywa unaleta matokeo chanya na kuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta
nyingine mtambuka na uchumi kwa ujumla wake.
Amesema kuwa ongezeko la ndege na huduma za usafiri inasaidia
kuongeza fursa za biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine kuongeza
upatikanaji wa fedha za kigeni na kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini.
Amesema hayo leo (Jumanne, Machi 26, 2024) alipomuwakilisha
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing
737-9 Max, kwenye uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ili kuendelea kuikuza
sekta ya anga nchini, Wizara ya Uchukuzi iandae mpango wa kuongeza wataalamu
wazalendo katika fani zinazohusu masuala ya ndege hususan katika eneo la
matengenezo na urubani.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa Shirika
la Ndege Tanzania kuongeza uzalendo na kuwafichua wale wote wenye nia ya
kulihujumu shirika hilo pamoja na kudhibiti upotevu wa mapato kupitia tiketi na
mizigo.
Pia, amewataka viongozi na watendaji wa Shirika hilo
wahakikishe ndege zote zinaendeshwa kwa tija kwa kufanya tafiti za kutosha wa masoko kabla ya kupeleka ndege.
Amesema kuwa usafiri wa anga umekuwa chachu ya kuongeza
mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo na biashara. “Uwepo wa usafiri wa ndege
umeongeza tija kubwa kwa wakulima hususan wa mazao ya mbogamboga na matunda,
wafugaji na wafanyabiashara wa Kitanzania.”
Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema katika
kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya sita imesaini mikataba ya miradi
mipya 6 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 674.3 inayohusu ujenzi wa kiwanda cha
kujengea meli (shipyard) katika Ziwa Tanganyika, ujenzi wa meli kubwa ya kubeba
mizigo tani 3,500 na meli nyingine yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 za mizigo
ambayo inajengwa katika Ziwa Victoria.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa
amesema kuwa sambamba na ununuaji wa ndege za abiria na moja ya mizigo,
Serikali imenunua ndege mbili za mafunzo kwa ajili ya Chuo cha
Usafirishaji (NIT) ili kusaidia kuongeza idadi ya marubani kwenye soko
la ajira na kupunguza uhaba wa marubani nchini.
“Pia NIT imewezesshwa mitambo na vifaa vya kisasa kwa ajili
ya kutoa mafunzo ya shahada na Stashahada ya uhandisi wa ndege ili kuzalisha
wahandisi na mafundi mchundo watakaoingia kwenye soko la ajira.”
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL)
Mhandisi Ladislaus Matindi amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kuendelea kuijengea kampuni hiyo uwezo wa kutoa huduma kwa kuinunulia ndege
mpya na kuijengea miundombinu wezeshi katika biashara ya anga.
“Hadi sasa Serikali imewekeza shilingi trilioni 2.4 katika
ununuzi wa ndege, ujenzi wa mindombinu wezeshi ya kibiashara pamoja na ulipaji
wa sehemu ya madeni yaliyolimbikizwa.”
Ameongeza kuwa ATCL inaendelea kutekeleza mpango mkakati wake
wa pili wa miaka mitano ulioanza mwaka wa fedha 2022/23 na kumalizia 2026/27
ambao pia unahusisha mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano yaani
2021/22-2025/26 ambao unatarajiwa kuiwezesha ATCL kuwa na ndege 20 “Hadi sasa
ATCL inandege 14 zilizonunuliwa katika kipindi cha ufufuaji.”
Ndege mpya aina ya B737-9 MAX ikipewa heshima ya kumwagiwa
maji (Water Salute) baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere jijini Dar es Salaam Machi 26, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu).
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni