Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA) Richard Kiiza amefanya ziara katika baadhi ya vijiji vilivyoko ndani ya
hifadhi ya Ngorongoro kukagua maendeleo ya timu ya uelimishaji na uandikishaji
wa wananchi wa tarafa ya Ngorongoro wanaojiandikisha kuhama kwa hiari ndani ya
hifadhi hiyo.
Akiwa kwenye ziara katika Vijiji vya Kayapusi na Oloirobi
vilivyopo kata ya Ngorongoro, Kamishna Kiiza amekutana na moja ya timu
inayoendelea na zoezi la uandikishaji na kuelezwa kuwa wananchi wameendelea
kuhamasika na kujiandikisha kwa hiari hasa baada ya kupata elimu ya faida na
hasara za kuishi ndani ya hifadhi na kupata taarifa za fursa lukuki za ndugu
zao waliokwisha hama ndani ya hifadhi.
Akizungumza na baadhi ya wananchi aliokutana nao Kiiza amewaeleza
kuwa Serikali hailazimishi mtu kuhama isipokuwa inamuelimisha hasara za kuishi
ndani ya hifadhi ambapo sheria inazuia kufanya baadhi ya vitu ukilinganisha na
mazingira anakoenda ambapo serikali imeboresha mazingira kwa kujenga
miundombinu ya maji, shule, barabara, umeme, mawasiliano, eneo la malisho,
minada na soko la maziwa.
Ameongeza kuwa wananchi ambao wangependa kwenda kuona maeneo
yaliyoandiliwa na Serikali kabla ya kuamua kuhamia wana uhuru wa kufanya hivyo
ili kukagua maeneo yaliyoandaliwa katika vijiji vya Msomera, Kitwai na Saunyi
na serikali ipo tayari kuwapa ushirikiano.
“Serikali haiwezi kuwa na nia mbaya kwa watu wake, ndio maana
inajenga miundombinu yote muhimu, inawapa wananchi wanaohama fedha za motisha
zinazotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan, sambamba na kuwapa fidia ya maendelezo waliyofanya wakiwa ndani ya
hifadhi na kuwahamishia thamani na mifugo yao yote kwenda maeneo waliyochagua kwa
kufuata misingi ya sheria, kanuni na haki za binadamu,” amefafanua Kiiza.
0 Maoni