Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA) Richard Kiiza ameendelea na ziara ya kukagua zoezi la uelimishaji,
uandikishaji na uthaminishaji wa mali za wananchi wa Ngorongoro wanaoendelea
kuhamasika na kujiandikisha kuhama kwa hiari ndani ya hifadhi.
Wananchi hao wameendelea kuhamasika kuhama kwa hiari kwenda
nje ya hifadhi hasa Kijiji cha Msomera na maeneo mengine waliyochagua wenyewe
kwa lengo la kupisha shughuli za uhifadhi na kwenda maeneo ambayo serikali
imewajengea miundombinu ya kisasa kama shule, maji, barabara, zahanati, umeme,
mawasiliano, huduma za posta, majosho, malisho na mashamba ya kilimo.
Mtendaji wa Kijiji cha Kapenjiro kata ya Naiyobi Mejisho
Mollel amemueleza Kamishna Kiiza kuwa hadi sasa katika Kijiji chake zaidi ya
kaya 235 zimeshajiandikisha kuhama katika Kijiji hicho na muamko wa wananchi
wanaotaka kuhama umeendelea kuwa mkubwa kadri siku zinavyoenda.
Diwani wa Kata ya Naiyobi tarafa ya Ngorongoro Mhe. Ngeresa
Reteti anaeleza kuwa wananchi wa kata hiyo wameendelea kuhamasika kujiandikisha
kuhama hasa baada ya Serikali kuweka utaratibu mzuri wa wananchi kujiandikisha
kwenye Ofisi za Kijiji na kuhakikisha kuwa wanaoandikishwa na kufanyiwa
tathmini ya mali zao wanahamishwa ndani ya muda mfupi bila kukaa muda mrefu.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Richard Kiiza
anabainisha kuwa kwa sasa Serikali imeboresha utaratibu wa kuelimisha na
kuwaandikisha wananchi kwa kuwafuata sehemu walipo na zoezi la kuwaandikisha
linapokamiliaka malipo huandaliwa haraka na ndani ya siku zisizozidi 10 taratibu zinakuwa
zimekamilishwa na mwanachi kuhamishwa yeye na mifugo yake na kulipwa stahiki
zake zote.
“Tunahakikisha kuwa mwananchi akiijiandikisha na
kuthaminishiwa mali zake, ndani ya siku kumi (10) taratibu zote ikiwepo malipo
zinakamilishwa ili mwanachi ahamishe bila kuchelewa, kwa sasa tumeongeza timu
ya wataalam kutoka chou cha maendeleo ya Jamii ili kuwafikia kwa haraka
wananchi wanaotaka kujiandikisha bila kuwachelewesha,” amefafanua Kamishna
Kiiza.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA) Richard Kiiza akiongea na baadhi ya wanakijiji cha Kapenjiro kata ya Naiyobi,
waliohamasika kuhama kwa kwenda nje ya hifadhi hasa Kijiji cha Msomera na
maeneo mengine waliyochagua wenyewe.
0 Maoni