Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania - TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko amewataka Maofisa
na askari wa Mapori ya akiba Ikorongo na Grumeti kuongeza umahiri katika
utendaji kazi ili kuendana na kasi ya uwekezaji mahiri (SWICA) uliofanyika
ndani ya hifadhi hizo zilizoko wilaya za Serengeti na Bunda Mikoa ya Mara na
Simiyu.
Semfuko ameyasema hayo Machi 06, 2024 wakati wa ziara ya siku
moja ya kutembelea na kujionea shughuli zinazofanywa na TAWA katika hifadhi
hizo.
Akizungumza na Maafisa na askari wa Mamlaka hiyo katika eneo
la Fort Ikoma, Mwenyekiti huyo aliwasisitiza kuongeza ushirikiano kati ya TAWA
na wawekezaji ikiwemo Kampuni ya Grumeti Fund Trust katika kuhakikisha shughuli
za uhifadhi zinaimarishwa.
Alisema Bodi kwa kushirikiana na Serikali wameendelea kufanya
maboresho makubwa ndani ya Mamlaka hiyo kwa kuboresha mazingira ya utendaji
kazi wa watumishi hasa kuongeza vitendea kazi.
“Kipindi cha nyuma TAWA ilikuwa katika mazingira magumu,
Askari wetu walifanya kazi kubwa lakini hawakuwa na vitendea kazi, lakini kwa
sasa tumefanya maboresho makubwa, na maboresho haya lazima yaendane na nyie
kuwa na nidhamu kubwa,” alieleza Mej. Jen. (Mstaafu) Semfuko.
Kwa upande wake Prof. Suzana Augustino, Mjumbe wa Bodi hiyo,
alisisitiza kuhusu matumizi ya teknolojia katika utekelezaji wa majukumu ya
Mamlaka hiyo hasa shughuli za uhifadhi ikiwemo ujangili na wanyama vamizi.
Prof. Suzana alisema teknolojia itarahisisha shughuli za
uhifadhi kwenda kwa haraka na kwa wakati, kwani dunia kwa sasa imebadilika na
ipo katika kipindi cha sayansi na teknolojia.
Kaimu Naibu Kamishna wa uhifadhi (TAWA) Mlage Kabange, ambaye
alimuwakilisha Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda, alisema
Mapori ya akiba manne yaliyopo chini ya Mamalaka hiyo katika Kanda ya Ziwa,
yamekuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa.
Alisema Mapori hayo yamekuwa na shughuli mbalimbali za utalii
wa picha, na utalii wa uwindaji, ambapo mchango wake kwenye mapato ya Mamlaka
ni takribani asilimia 25.
“Haya Mapori ya Akiba manne yaliyopo Kanda ya Ziwa, ni kati ya Mapori ya kimkakati
ya Mamlaka. Yamekuwa na mchango mkubwa kwenye pato la Taifa, na tunaendelea
kuboresha mazingira ya utekelezaji wa shughuli za uhifadhi kwenye mapori haya,”
alisema Kabange.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali
za Mamlaka hiyo, Kaimu Kamanda wa Uhifadhi (TAWA) wa Kanda ya Ziwa Said Kabanda
alisema katika kupambana na ujangili katika kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi
Desemba 2023 jumla ya mitego ya yaya 4,088 ilikamatwa kupitia doria 97,565
zilizofanywa na askari wa Mamlaka hiyo kwenye mapori hayo.
Aliongeza kuwa katika kipindi hicho jumla ya majangili
waliokamatwa walikuwa 1,120 na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa
mahakamani.
0 Maoni