Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), umeanza
kutoa mafunzo ya siku tatu kwa wawakilishi kutoka nchi za Burundi na Sudan
Kusini juu ya utoaji wa huduma za Urasimishaji wa biashara kwa njia ya mtandao
katika Ofisi za taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam.
Akifungua mafunzo hayo jana , Kaimu Mkurugenzi Idara ya
Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Sempeho
Manongi, akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara amesema kuwa lengo
la mafunzo hayo ni kuwafundisha wawakilishi hao namna ya kutumia mifumo ya
Usajili ili wakatumie ujuzi huo katika kuanzisha na kuendeleza mifumo kwenye
nchi zao.
“Katika moja ya mambo makubwa ambayo Serikali imefanya ni
kuunganisha mfumo mmoja wa kuwezesha kusajili biashara na kupata Leseni,
uliowezesha kufanya vizuri zaidi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kupelekea nchi ya Sudan Kusini na Burundi kuja kujifunza,” amesema Bw. Manongi.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey
Nyaisa amefurahishwa na ujio wa ugeni huo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa
kwa kuiona Tanzania kupitia taasisi ya BRELA kuwa imepiga hatua upande matumizi
ya mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao hii inaonesha wazi kuwa kazi kubwa
inafanyika katika uwezeshaji na urasimishaji wa biashara nchini.
“Sisi tutawapitisha na kuwaonesha mifumo yetu hatua kwa hatua
namna mfanyabiashara anavyosajili hadi afisa anavyochakata maombi mbali na hayo
tunatarajia kutengeneza mashirikiano ya kufanya kazi ili sisi katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki tuweze kuongea lugha moja,” amesema Bw.Nyaisa.
Naye Mwakilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
anayeshughulikia Uwekezaji Bw. Charles Omusama amesema nchi hizi mbili zipo
kwenye machakato wa kuanza kutoa huduma za usajili kwa njia ya mtandao hivyo
Tanzania imeonekana ni nchi iliyopia hatua katika utoaji wa huduma kwa kutumia
mifumo.
Aidha, Kaimu Msajili Mkuu wa Kampuni za Biashara kutoka
Wizara ya Sheria Sudan Kusini Bw.Madol Anyuat amesema kuwa wapo Tanzania kwa
ajili ya ziara ya mafunzo kwa vitendo ili waweze kuona namna mifumo ya sajili
inavyofanya kazi ili watakaporudi watachukua hatua ya kuanzisha mifumo ya
kusaidia ukuaji wa sekta ya biashara.
Naye Bi.Alida Mugisha, ameeleza kuwa nchi ya Burundi imeanza
kutumia mifumo ya usajili mwaka 2022 ila bado wanakumbana na changamoto
mbalimbali, kwa kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa hivyo ziara hii itawajengea
uwezo ili waboreshe katika nchi yao.
Mafunzo haya yaliyoanza leo yanatarajiwa kufanyika kwa muda
wa siku tatu yatakwenda sambamba na mafunzo kwa njia ya vitendo pamoja na
kutembelea wadau wakubwa wanaotumia huduma za BRELA.
0 Maoni