WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Sekta ya elimu ni
wakala wa mabadiliko katika jamii kiuchumi, kiteknolojia na kiutamaduni katika
kuleta maendeleo ya nchi.
Amesema kuwa utoaji wa elimu bora kwa Watanzania ni moja ya
vipaumbele vya nchi katika kuleta maendeleo. “Ili kufanikisha haya tunahitaji
sekta hii kuwa bora, imara, inayokidhi mahitaji ya jamii kwa kuwapa vijana
maarifa na ujuzi wa kukabiliana na matatizo ya kijamii, kitaifa na kimataifa”.
Amesema hayo jana Machi 25, 2024 wakati wa mkutano wa wadau
wa Sekta ya Elimu mkoani Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha
Biblia-TAG jijini Dodoma.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Suluhu
Samia ni mdau namba moja wa sekta ya elimu na ndio maana katika kipindi cha
miaka mitatu ya uongozi wake amewekeza katika kuweka mazingira bora ya utoaji
elimu na kuhakikisha Serikali inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya
maendeleo katika Sekta ya Elimu.
“Ninaamini sisi sote ni mashuhuda wa jinsi Mheshimiwa Dkt
Samia Suluhu Hassan, katika kipindi cha uongozi wake alivyotekeleza kwa vitendo
azma ya kuhakikisha elimu bora inapatikana kwa Watoto wote wa Kitanzania bila
kujali jinsia wala hali ya kiuchumi.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa baadhi ya maeneo ambayo Rais
Dkt. Samia ameyasimamia kikamilifu ni Mpango wa Uboreshaji wa Miundombinu ya
Elimu, Ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi, Mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu,
Mapitio ya Sera Ya Elimu na Mafunzo.
Maeneo Mengine ni Kuimarisha Usimamizi wa Sekta ya Elimu kwa
kutoa vyombo vya usafiri kwa viongozi wasimamizi wa elimu pamoja na wathibiti
ubora wa shule, Kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji Elimu na kutoa
Mafunzo kwa walimu kazini (MEWAKA) kwa ajili ya kuwajengea uwezo na umahiri
katika kutimiza majukumu yao.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amewataka viongozi
katika halmashauri nchini kuhakikisha fedha zinazoletwa kwa ajili ya kulipa
stahiki mbalimbali za walimu zisipangiwe matumizi mengine. “Walimu wapewe
stahiki zao mara moja ili kuondoa malimbikizo ya madeni yasiyo ya lazima na
manung’uniko dhidi ya Serikali bila sababu.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Maafisa elimu nchini
kuwa na utaratibu wa kwenda vijijini ili kubaino changamoto katika sekta hiyo
badala ya kukaa ofisini pekee.
Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule
amesema kuwa katika kipindi cha Miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kiasi cha Shilingi bilion 92.4 zimetolewa kwa ajili miundombinu ya elimu mkoani
humo.
“Idadi ya shule za msingi za Serikali imeongezeka kutoka 784
mpaka kufikia shule 819 mwaka 2023/2024, wakati shule za Sekondari zimeongezeka
kutoka 218 mpaka kufikia 235”.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni