Amchinja mkewe shingoni kisa wivu wa mapenzi

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Ombeni Manase Kilawa (43) mkazi wa Lusese Wilaya ya Mbarali kwa tuhuma za kumuua mke wake aitwaye Happynes Gervas Mwinuka (40) mkazi waKijiji cha Lusese kwa kumkata na kitu chenye nchakali.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Machi 13, 2024 Kitongoji cha Masista, Kijiji cha Lusese, Wilaya ya Mbarali baada ya kutokea ugomvi baina ya wanandoa hao wakiwa nyumbani kwao na kupelekea mtuhumiwa Ombeni Kilawa kuchukua kisu na kumkata mke wake shingoni.

Akiongelea tukio hilo leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP Benjamin Kuzaga amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi baada ya mtuhumiwa kumhisi na kumtuhumu mkewe kuwa na mahusiano ya mapenzi na wanaume wengine.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, limetoa wito kwa jamii kuwa pindi wanapopatwa natatizo au changamoto katika ndoa zao isiwesuluhisho lake kujichukulia sheria mkononi bali ni kutafuta ushauri kwa wazazi, walezi, wasimamizi wa ndoa, viongozi wa dini, katika madawati yajinsia na watoto waliopo kila Wilaya ya Kipolisi, katika ofisi za halmashauri au kutafuta haki kwenye Mahakama ili kuepuka madhara.

Chapisha Maoni

0 Maoni