Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) umeishukuru
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan kutokana na uwekezaji uliofanyika hospitalini hapa ambao umewezesha
huduma mbalimbali za kibingwa na ubingwa bobezi kufanyika ikiwemo upasuaji
mkubwa wa kutenganisha watoto pacha.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuwaruhusu
watoto pacha waliozaliwa kwa nje wakiwa wameungana tumbo na kifua, ndani
waliungana ini na mfupa wa kidari, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Mohamed
Janabi, amesema uwekezaji wa kusomesha watalaam, kuboresha miundombinu na
ununuzi wa vifaa vya uchunguzi vya kisasa umeiwezesha hospitali hiyo kutoa
huduma zinazolingana na hadhi yake.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto MNH,
Dkt. Victor Ngota ameeleza kuwa upasuaji wa kuwatenganisha watoto hao,
ulichukua saa sita na kuhusisha jopo la wazawa lenye utaalam mchanganyiko wa
hali ya juu wa madaktari bingwa wa upasuaji watoto, upasuaji rekebishi,
usingizi na ganzi, watalaam wa lishe pamoja na radiolojia.
“Tuliwapokea watoto hawa tarehe 11 Machi 2023 wakiwa na
jumla ya kilo nne hivyo tulianza mchakato wa kuwahusisha wataalam ambao
wanahusika na huduma hizi, ilituchukua takribani muda wa miezi kumi kuangalia
mwenendo wao wa afya kwa ujumla kabla ya kuwatenganisha ili kuweza kupata dira
ya namna watakavyoishi mara baada ya kutenganishwa ambapo hadi wanatenganishwa
walikua na kilo 16 sawa na kilo nane kwa kila mmoja,” amefafanua Dkt. Ngota.
Mzazi wa watoto hawa Bi. Mariam Shabani, mkazi wa Kigamboni Jijini Dar es Salaam, ameishukuru Serikali na watoa huduma wote wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na jinsi alivyohudumiwa katika kipindi chote alichokuwa hapo.
0 Maoni