WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi
mkoa wa Mara, ACP Salum Morcase amkamate Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu
wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Bw. Saad Mutunzi Ishabailu kwa kosa la
kuhamisha sh. 213,748,085 kwa awamu nne kwa njia ya uhamisho wa ndani kwa
kushirikiana na watumishi wa OR TAMISEMI na kuzitumia kwa matumizi yao binafsi.
“Mkamate huyo bwana sasa hivi aende polisi akafunguliwe
mashtaka, huyu ni wa kupeleka mahakamani moja kwa moja. DPP aelezwe afungue
jalada la mashtaka. Wale wenzake tumewapeleka mahakamani tayari sababu
tulibaini walihusika na wizi kama huu kwenye Manispaa ya Kigoma mwaka jana.”
Ametoa agizo hilo leo jioni (Jumanne, Februari 27, 2024)
wakati akizungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Serengeti kwenye kikao kilichofanyika katika kwenye Halmashauri hiyo, mkoani
Mara.
Waziri Mkuu amefikia hatua hiyo baada ya kuwaeleza watumishi
na madiwani mbinu wanazotumia watumishi wachache wa baadhi ya Halmashauri ambao
walikuwa wanashirikiana na watumishi watatu wa kitengo cha Treasury Single
Account (TSA) kuiba fedha za umma.
Akitolea mfano juu ya mbinu zinazotumika na wachache hao,
Waziri Mkuu aliwaeleza watumishi wa Halmashauri hiyo pamoja na Madiwani kwamba
Juni 10, 2023 walitumia mwanya wa kuombea kibali fedha za bakaa kwa barua
iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Chatta Luleka, kwenda HAZINA.
“Ilipofika Juni 30, walikuwa wamemaliza kutumia fedha hizo
na ikabakia sh.milioni 9 lakini kwa kuwa walishaandika barua ya kuomba kibali,
bado fedha hizo zilihamishwa na kuingizwa kwenye akaunti ya Halmashauri tarehe
19 Juni 2023 na aliyejua alikuwa Bw. Ishabailu peke yake. Hakutoa tarifa kwa
Mkurugenzi, Mwenyekiti wala wakuu wa idara.”
“Nilituma timu yangu hapa ije kufanya uchunguzi, ikawahoji
baadhi ya watumishi akiwemo Afisa Mipango wa Halmashauri, Bw. Wilfred Mwita
ambaye alisema hajui uwepo wa hizo fedha wala hawakuwa na mpango wala bajeti
inayohitaji hizo fedha. Mkurugenzi wa sasa, Bw. Furaha alipoulizwa naye alisema
hajui uwepo wa hizo fedha, kwani alianza kazi Agosti, mwaka jana.”
Amesema Juni 21, mwaka jana Bw. Ishabailu alianza kufanya
matumizi ya hizo fedha kwa kushirikiana na mfanyabiashara wa hapa Mugumu, Bw.
Daudi Matinde Chacha kupitia kwenye akaunti zake za NMB na CRDB kwa kupitia
miamala minne ya sh. milioni 76.3, sh. milioni 57.7, sh. milioni 47 na
sh.milioni 32.5.
Amesema alipoulizwa na timu ya uchunguzi Bw. Matinde alikiri
kuwa haidai fedha yoyote Halmashauri ya Serengeti isipokuwa Mweka Hazina huyo
aliomba apitishie fedha zake kwenye akaunti zake kwa sababu zinahitajika haraka
kwa matumizi ya ofisi. “Aliambiwa atoe
shilingi milioni 189 akamkabidhi zote Bw. Ishabailu na zilizobakia (sh. milioni
24) akaambiwa abaki nazo,” amesema Waziri Mkuu.
“Baada ya kupokea fedha hizo, Bw. Ishabailu alipanda basi
kutoka Serengeti hadi Kituo cha Mabasi cha Nyegezi, Mwanza na kumkabidhi Bw.
Zablon Mponzi ambaye alisema zinatakiwa haraka na wakubwa huko Dodoma bila
kuwataja wakubwa hao ni akina nani. Yeye pia alikabidhi shilingi 150 kwa huyo
Zablon, ina maana alibakia na sh. milioni 39.”
Aliwasisitiza madiwani na watumishi wawe makini na matumizi ya fedha za umma kwani Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anapotafuta hizi fedha na kuzileta kwenye Halmashauri anataka zije kutatua kero za wananchi walio wengi. Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake wilayani Tarime.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni