Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amesema
kuwa Serilikali imeanza kuandaa mpango wa majadiliano ya namna ya kuzirejesha
malikale zilizopo katika Taifa la Ujerumani ambapo baadhi ya malikale hizo ni
kutoka katika Mkoa wa Ruvuma.
Waziri Mhe. Kairuki amesema haya katika hotuba ya Kilele cha
Tamasha la Kumbukizi ya Vita vya MajiMaji iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa
Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas katika Makumbusho ya MajiMaji, mjini Songea.
Mhe. Kairuki amesema kuwa wakati wa utawala wa Wajerumani
katika mkoa wa Ruvuma ziko Malikale nyingi zilizochukuliwa na kupelekwa Taifa
la Ujerumani na kwamba ni wakati muafaka sasa wa kuzirejesha ili Mkoa wa Ruvuma
na Tanzania kwa ujumla inufaike nazo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na
Utalii, Kamishna Benedict Wakulyamba
amesema kuwa Tamasha hili hutoa fursa kwa Wananchi kushiriki katika
kuhifadhi, kuenzi na kuendeleza uzalendo, amani na mshikamano vitu ambavyo ni
urithi kutoka kwa Mashujaa wa vita vya Majimaji lakini pia kuchochea na kuibua
vivutio vya Utalii vinavyopatikana katika Kanda ya kusini.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Makumbusho ya Taifa la
Tanzania, Bi.Mistica Ngongi amesema vita
vya Majimaji inawakumbusha nia thabiti ya Watanzania wa enzi hizo ya kuilinda
jamii yao, lakini pia inawakumbusha Watanzania tunu za uzalendo, ari, ujasiri,
uthubutu na umoja wao kwa maslahi makubwa ya Taifa la Tanzania.
Naye Chifu wa kabila la Wangoni Inkosi wa Makosi Zulu Gama
amesema ni muhimu kuendelea kuwaenzi mashujaa wa vita vya Majimaji kwa
kuwaombea kwa kuwa walishiriki kwa uaminifu kurithisha tunu ya amani na
uzalendo na maadili mema kwa kizazi kilichopo sasa.
Kilele cha Tamasha la Vita vya Majimaji hufanyika kila ifikapo 27 Februari kila mwaka ambapo lilitanguliwa na matukio mbalimbali ikiwemo mashindano ya ngoma za asili kwa halmashauri nane za Mkoa wa Ruvuma, Kongamano la Wadau kuhusu Kumbukizi ya Vita vya Majimaji na maadhimisho ya Siku ya Wangoni katika kijiji Cha Maposeni.
Yaz Nyirenda "Deputy Secretary General for Malawi Ngoni Heritage" akihamasishwa kutembelea vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji zinazopatikana ndani ya Hifadhi za Taifa 21 zinazopatikana Tanzania Bara na Afisa Uhifadhi Mwandamizi Seth Mihayo, alipotembelea Banda la TANAPA wanaoshiriki Tamasha la Kumbukizi la vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni leo tarehe 27/2/20204 katika Viwanja vya Mashujaa Songea Mkoani Ruvuma.
0 Maoni