Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeandaa
kikao cha mashauriano na Wadau kuhusu Sheria ya Kimataifa ya Shirika la Miliki
Ubunifu (World Intellectual Property - WIPO) itakayolinda Miliki Ubunifu katika
Rasilimali za Kijenetiki na Ujuzi wa Jadi kilichofanyika mwishoni mwa wiki,
Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey
Nyaisa amesema kuwa mashauriano hayo yanalenga kujadili na kuona namna bora
Nchi itakavyoweza kunufaika na Sheria hiyo ya Kimataifa ambayo ikikamilika italeta
manufaa kwa Nchi na Jamii za Kijadi kupitia Miliki Ubunifu zitakazotokana na
Rasilimali hizo.
Amesema kuwa katika Ulimwenguni huu wa Sayansi na Teknolojia
ni vyema bunifu zinazotokana na Rasilimali za Kijenetiki na Ujuzi wa Jadi
zikawaletea manufaa wamiliki hasa jamii ambazo rasilimali na ujuzi huo
unapatikana. Hivyo Sheria ya Kimataifa
kuhusu Ulinzi wa Rasiliamli hizo imekuja kwa muda muafaka ili kuzuia matumizi
yasiyo halali ya Rasilimali hizo kwa kuweka uwazi na kuwaletea faida wahusika.
Ameongeza kuwa, tiba za jadi au mbadala zimesaidia katika
kutoa kinga na tiba kwa magonjwa mengi hapa nchini ambapo toka enzi jamii
zimekuwa zikitumia tiba hizo, hii inathibitishwa na Ripoti ya Shirika la Afya
Duniani (WHO) ya 2019 ambayo inabainisha kuwa zaidi ya asilimia 79 ya
watanzania wanatumia tiba za jadi.
"Tunatambua kuwa Taifa letu limejaliwa kuwa na
rasilimali nyingi za kijenetiki zitokanazo na mimea, wanyama na ujuzi wa jadi
ambavyo vina thamani ambayo wengi hawafahamu na mara nyingine rasilimali hizo
kutumiwa na watu wengine pasipo kuwaletea manufaa wahusika. Kwa sasa tumejipanga kusaidia wabunifu
waweze kulinda bunifu zao na baada ya ulinzi wafaidike na bunifu hizo, na
matumizi ya rasilimali hizi yawe na faida kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa
ujumla," amedokeza Bw. Nyaisa.
Amepambanua kuwa Jamii yetu imekuwa na watafiti mbalimbali
na wataalamu ambao hubuni vitu mbalimbali ikiwepo dawa za jadi ambazo
zikilindwa na kutumika ipasavyo zinaweza kuwapatia wamiliki wa bunifu hizo
manufaa makubwa.
Akitoa wasilisho kuhusu Sheria ya Kimataifa ya WIPO juu ya Miliki Ubunifu katika Rasilimali za Kijenetiki na Ujuzi wa Jadi, Kaimu Mkurugenzi wa Milki Ubunifu kutoka BRELA Bi. Loy Mhando amesema kuwa kupitia Sheria hiyo nchi wanachama za WIPO ikiwemo Tanzania, zitafaidika na bunifu zitokanazo na Rasilimali za Kijenetiki na Ujuzi wa Jadi kutoka katika Nchi hizo.
Sheria hii itazuia matumizi ya rasilimali hizo pasipo
kufichua mahali zinapopatikana na kuhakikisha jamii husika zinapata faida
itokanayo na matumizi ya rasilimali hizo, watalindwa na kupewa haki ya kipekee
katika matumizi ya rasilimali hizo.
Kwa kuhutimisha amesema kuwa majadiliano ya Sheria hiyo yatazaa Itifaki ambayo itakamishwa mwezi Mei 2024 katika mkutano wa kidplomasia utakaofanyika makao makuu ya WIPO Jijini Geneva, Uswisi.
Kaimu Mkurugenzi wa Milki Ubunifu kutoka BRELA Bi. Loy Mhando akizungumza kwenye kikao cha mashauriano na Wadau kuhusu Sheria ya Kimataifa ya Shirika la Miliki Ubunifu (World Intellectual Property - WIPO) itakayolinda Miliki Ubunifu katika Rasilimali za Kijenetiki na Ujuzi wa Jadi kilichofanyika Jijini Dar es Salaam.
0 Maoni