Viongozi wa Juu wa Serikali kushiriki mazishi ya Lowassa

  

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Jumamosi ya tarehe 17 Februari, 2024, atawaongoza maelfu ya Watanzania na viongozi mbalimbali kwenye mazishi ya Waziri Mkuu mstaafu, Hayati Edward Ngoyai Lowassa, yatakayofanyika kijijini kwake Ngarash, wilayani Monduli, mkoani Arusha.

Akiongea na waandishi wa habari Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Mobhare Matinyi amesema pamoja na Mhe. Rais viongozi wengine wa kitaifa watakaohudhuria ni Mhe. Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango, Mhe. Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi; Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa; Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.

 Aidha, viongozi wengine wa kitaifa watakaokuwepo ni pamoja na Mhe. Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Dotto Mashaka Biteko; Mhe. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Mungano, Dkt. Tulia Ackson; Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Zubeir Ali Maulid, na viongozi wastaafu wa Serikali ya

Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; na hali kadhalika mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa vyombo vya dola, wakuu wa taasisi za umma na binafsi na watendaji wengine.

Amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitawakilishwa na safu ya juu ya uongozi wake ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Komredi Abdulrahman Omar Kinana. Hali kadhalika, vyama vya upinzani nchini vinatarajiwa kutuma uwakilishi wa ngazi za juu katika mazishi hayo. 

Bw. Matinyi ameeleza kuwa Kamati ya Kitaifa ya Mazishi chini ya mwenyekiti wake, Mhe. Waziri

Mkuu Majaliwa, inaendelea kukumbushia kwamba siku ya Ijumaa ndiyo itakayokuwa siku rasmi kwa waombolezaji wote kutoa heshima zao za mwisho na kuacha siku ya Jumamosi kwa ajili ya familia na viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia kufanya hivyo pia. 

Amesema viongozi wa kimila, Laigwanan, watapata fursa ya kutoa heshima za mwisho na salamu za rambirambi siku ya Ijumaa.

Bw. Matinyi amesema Ibada takatifu ya mazishi Jumamosi, Februari 17, itaongozwa na Kanisa la

Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT); na kwa kuzingatia kwamba haya ni mazishi yenye hadhi ya kiserikali, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ndilo linaloshughulikia taratibu za mazishi ya heshima za kijeshi ikiwemo kupiga mizinga 17 wakati mwili utakapoteremshwa kaburini.

Chapisha Maoni

0 Maoni