Inakadiriwa kuwa takribani watu milioni 50 duniani wana
ugonjwa wa kifafa na wengine wapya milioni sita wanagundulika kila mwaka ambapo
nchini Tanzania kuna wagonjwa zaidi ya milioni moja wanaokabiliwa na tatizo
hilo.
Hayo yameelezwa leo na Mganga Mkuu wa
Serikali, Prof. Tumaini Joseph Nagu wakati akizungumza kwenye kongamano la
maadhimisho ya siku ya kifafa duniani lililoandaliwa na Chama cha Watalam wa
Kifafa Tanzania (TEA) na kuadhimishwa leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
ambapo ameitaka jamii kuacha tabia ya kuwaficha wagonjwa wenye kifafa kwakuwa
wagonjwa hawa wakitumia dawa wanaweza kuishi kama watu wengine.
Ameongeza kuwa pamoja na kwamba ugonjwa huu umeanza siku
nyingi bado jamii inaendelea kuhusisha na imani potofu na kuwaficha watoto wenye
ugonjwa huo ndani na kuwasababisha kukosa huduma za matibabu mapema.
“Mtu mwenye ugonjwa wakifafa akichelewa kupata matibabu
anaweza kupoteza maisha mapema kutoka na madhara mbalimbali ikiwemo kudondoka
sehemu zenye hatari ikiwemo kwenye moto au kugongwa na gari,” amesemea Prof.
Nagu.
Pamoja na hayo amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya
inaendelea kuongeza vituo vya kutolea huduma na kuweka dawa muhimu ili
kupunguza uwezekano wa mtoto anayezaliwa kupata ugonjwa wa kifafa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TEA,
Prof. William Matuja amesema kuwa ugonjwa wa kifafa unasababishwa na magonjwa
yanayoshambulia ubongo hasa wakati mtoto anapozaliwa, mtoto kupata ugonjwa wa
degedege unaojirudia, malaria kupanda kichwani au kula vyakula vyenye vijidudu.
“Leo tunakumbushana na kuelemishana kuwa ugonjwa huu unatibika na hauambukizwi kwakuwa ni ugonjwa unaonzia kwenye ubongo pia jamii itambue kuwa kifafa kinatibiwa na dawa za hospitali na kwa sasa kila kituo cha afya kinatoa huduma kwa watu wenye ugonjwa huu,” amesema Prof. Matuja.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi amesema kwa sasa kuna mabadiliko katika matibabu hivyo ni vyema wataalam kwenda sambamba na mabadilko hayo, pia amewataka kutumia kongamano hilo kujadili na kubadilishana uzoefu hasa katika maswala ya tiba.
0 Maoni