Siku Ya Kakakuona Duniani; Ujumbe Muhimu Kwa Jamii

 

Kila tarehe 17 Februari, dunia inashangilia siku ya kakakuona duniani. Lengo la kuweka siku hii ni kutukumbusha umuhimu wa wanyama hawa na wajibu wetu kama jamii katika kuwafanya wanyama hawa waendelee kuwepo kwa vizazi vingi vijavyo.

Kakakuona ni wanyama wa kipekee sana, upekee wao unatokana na sifa nyingi ambazo zinatofautiana na wanyama wengine tunaowafahamu. Ni moja ya wanyama ambao hawaonekani mara kwa mara, kutoonekana kwa kakakuona imepelekea mnyama huyu kuonekana wa ajabu.

Kakakuona ni mamalia pekee mwenye magamba, mwili wote wa kakakuona umefunikwa na magamba magumu, magamba hayo hufanya kazi ya ulinzi. Kakakuona anapokutana na hatari au adui yake huwa na tabia ya kujikunja na kuwa kama mpira, kwa kufanya hivyo hujilinda na maadui au hatari.

Sehemu za chini ya tumbo la kakakuona hakuna magamba, hivyo anapojikunja na kuwa kama mpira sio rahisi kwa adui yake kumshambulia au kumjeruhi.

Kutokana na maumbile yao ya kipekee, kakakuona wamekuwa wakioteka sana hisia za watu wengi pale anapoonekana, wengi wanasema endapo kakakuona anapoonekana ni ishara ya bahati, baraka, pia anaweza kutabiri matukio ya siku zijazo. Licha ya mambo haya kufanyika sehemu nyingi Tanzania, hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibishisha hayo mambo kama ni kweli.

Kakakuona ni wanyama wanaokula wadudu aina ya mchwa na siafu. Kakakuona mmoja anaweza kula zaidi ya wadudu milioni 70 kwa mwaka, hii ni idadi kubwa sana ya wadudu wanaoliwa na kakakuona, pia inaashiria umuhimu wao katika kuweka sawa mifumo ya ikolojia.

Spishi zote 8 za kakakuona zilizopo duniani zipo katika hatari kubwa ya kutoweka kutokana na biashara haramu, matumizi ya chakula, uharibifu wa mazingira yake, na ujangili. Hivyo nchi ambazo zina wanyama hawa zinatakiwa kuwa msitari wa mbele katika kutoa elimu na kuhifadhi wanyama hawa. 

Tanzania kuna aina 3 za kakakuona, ambao ni Giant ground pangolin au kakakuona mkubwa kuliko wote, mwingine anaitwa Termmincks ground pangolin au kakakuona wa ardhini, ambaye yupo maeneo mengi ya nchi ya Tanzania, na mwingine anaitwa White bellied pangolin au kakakuona mwenye tumbo jeupe, pia anaitwa tree pangolini, yaani kakakuona anayepanda miti.

Kakakuona wote watatu wanapatikana Tanzania, lakini cha kushangaza watu wengi hawajui na hudhani yupo mmoja tu. Lakini pia kakakuona hawa wanafanana sana, na sio rahisi kuwatofautisha kwa haraka.

Uwepo wa kakakuona hawa watatu hapa Tanzania ni ishara nzuri sana kwa uhifadhi na kwa dunia kwa ujumla. Hii inamaanisha Tanzania kuna mazingira mazuri ya wanyama hawa kuishi na kushamiri. Hivyo tunahitaji kuwajua kakakuona wa Tanzania na kuwahifadhi ili waendelee kuwepo kwa miaka mingi ijayo.

Lengo la kuandika makala hii ni kutaka uma na jamii nzima ya Tanzania kufahamu uwepo wa kakakuona katika nchi yetu, na nafasi yetu kama jamii kushiriki katika uhifadhi wa wanyama hawa wa ajabu.

Kakakuona ni wanyama wanaotembea zaidi usiku, na wakati mwingine mchana. Katika harakati za kutafuta chakula au kuwatafuta wenzao hujikuta wakiwa katika makazi ya watu, na hivyo watu wamekuwa wakitoa taarifa za kuonekana kwao maeneo mbali mbali.

Hii inamaanisha kuwa kakakuona anaweza kuonekana au kuja kwenye makazi ya watu, hivyo tunatakiwa kutoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya kijiji pia unaweza kutoa taarifa kwa watu wa maliasili waliuopo kwenye eneo ulilopo, au unaweza kutoa taarifa polisi.

Utoaji wa taarifa ni muhimu sana endapo kakakuona ameonekana kwenye maeneo yetu. Hii itasaidia usalama wa kakakuona huyo na pia usalama wako.

Kuna watu wakimuona kakakuona wanaenda moja kwa moja kwenda kumshika na kumsumbua sumbua, jambo hili sio zuri, maana wanyama hawa wanaweza kuwa na vimelea vya magonjwa hatari ya kuambukiza, pia unaweza kuwaambukiza magonjwa ambayo yanaweza kuwa hatari kwa kakakuona na wanyama wengine wa mwituni.

Njia nzuri ni kutoa taarifa kwa watalamu au watu wa maliasili kama vile TANAPA, TAWA, TFS, nk. Ili waje kumchukua na kumpeleka sehemu sahihi ambayo ina maji, mchwa na chakula chake.

Jambo jingine unaloweza kufanya endapo kakakuona ameonekana kwenye makazi yetu, usimpigie makelele, usimrushe rushe. Ikitokea umemshika au kumbeba kwa ajili ya kumpeleka sehemu husika unatakiwa kutumia nguo nzito, na kumuweka kwenye box zuri lenye hewa na unaweza kuweka hiyo nguo chini ili anaposafirishwa asiumie au kijigonga kwenye vitu kugumu akaumia na kujeruhiwa.

Endapo kakakuona ameonekana kwenye maeneo yenu, usimfiche au usikae naye muda mrefu bila kutoa taarifa kwa wahusika hii itasaidia kunusuru afya yake.

Kwasababu kakakuona ni mnyama mwenye aibu sana, sio rahisi kula au kuwa huru mbele za watu. Kuna wengine wakimuona kakakuona wanampa vitu mbali mbali kama unga, maji kama chakula, lakini tafiti zinaonyesha kuwa kakakuona hawezi kula mbele za watu kwa kuwa ni mnyama mwenye aibu sana.

Endapo utakutana na kakakuona kwenye makazi yake huko porini, ni vizuri ukamuacha huko huko porini alipo, usimchukue na kumpeleka kijijini au kwenda kumhifadhi kwako, jambo hilo ni hatari, na ni kosa kisheria. Soma zaidi makala hii kufahamu mengi kuhusu kakakuona wa Tanzania Spishi za Kakakuona wa Tanzania, na Mengi Usiyoyajua kuhusu Wanyama Hawa

Kuna mengi sana hayajulikani kuhusu kakakuona wa Tanzania, hivyo ni vizuri tukaweka nguvu kubwa kufanya tafiti za kina zinazoweza kutoa taarifa muhimu za kakakuona waliopo Tanzania. Kuna ukosefu mkubwa wa taarifa za idadi yao, maeneo halisi waliyopo, biashara na mitazamo ya jamii kuhusu wanyama hawa.

Jambo la kutia moyo ni kwamba, kuna taasisi isiyo ya kiserikali inayoitwa Tanzania Rsearch and conservation Organization (TRCO), ambayo ofisi zao zipo Morogoro mjini, wameanza kuonyesha mwanga katika kuwafuatilia kakakuona wa Tanzania ili kupata taarifa muhimu za kina ambazo zitasaidia katika uhifadhi wa wanyama hawa wazuri.

TRCO, kwa kushirikiana na serikali, wadau wa uhifadhi na wafadhili wa miradi yao, wamekua msitari wa mbele katika kutafiti maeneo yote muhimu yanayodhaniwa kuwa na wanyama hawa muhimu, lengo ikiwa ni kupata taarifa zote muhimu za kakakuona wa Tanzania, ambazo zitasaidia katika uhifadhi wa wanyama hawa hapa Tanzania.

Hivyo, basi katika kuadhimisha siku ya kakakuona duniani, niwaombe watu wote tushiriki katika uhifadhi wa mnyama huyu wa kipekee.

Imeandikwa na Hillary Mrosso, +255 683 862 481, hmconserve@gmail.com

Chapisha Maoni

0 Maoni