SERIKALI imedhamiria kuyafanya makazi ya hayati Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yaliyoko kijiji cha Mwitongo, wilayani
Butiama mkoani Mara kuwa kituo cha utalii.
Hayo yalisemwa jana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati
akizungumza na wakazi wa Kitongoji cha Muhumba, wilayani Butiama, akiwa njiani
kuelekea Mugumu, Serengeti ambako anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani
Mara.
Waziri Mkuu Majaliwa alimwagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Moses
Kaegele atembelee eneo, akagua na kuangalia mapungufu yaliyopo ili Serikali
iweze kuyafanyia kazi. Pia ameiagiza wizara ya ujenzi ishughulikie barabara ya
kutoka Serengeti hadi Butiama ili ikamilike na kuwawezesha watalii wanaotaka
kufika kwenye makumbusho hayo kwa njia ya barabara.
Waziri Mkuu alipitia Mwitongo na kuwasalimia wanafamilia wa
Baba wa Taifa na kuweka shada la maua kwenye kaburi lake.
Mapema, alipowasili wilayani humo, Waziri Mkuu aliweka jiwe
la msingi la ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama ambayo utekelezaji
wake umefikia asilimia 60.
Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe hilo, Waziri Mkuu
alimtaka mkandarasi wa mradi huo ambaye ni Wakala wa Majengo (TBA) ahakikishe anaukamilisha
mradi huo kwa wakati. Hadi sasa, mkandarasi ameshalipwa sh. milioni 843.4 ikiwa
ni malipo ya awali na hati za malipo ya pili na tatu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema Serikali kupitia
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na kazi ya kupeleka umeme kwenye
vijiji ambapo kazi kubwa imefanyika na sasa nguvu kubwa inaelekezwa kwenye
kufikisha umeme kwenye vitongoji.
Akizungumza na wakazi wa Issenyi, wilayani Serengeti, akiwa njiani kuelekea Mugumu, Mheshimiwa Majaliwa alitoa rai kwa Watanzania waachane na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake waanze kutumia gesi.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni