Imeelezwa kuwa ili Tanzania iweze kufikia malengo ya Maendeleo
iliyojiwekea, lazima iwe na Sera Bora ya Mambo ya Nje inayozingatia maoni na
matakwa ya makundi yote ya wadau nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Ikulu
Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika Kongamano
la wadau la kukusanya maoni kuhusu marekebisho ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya
Mwaka 2001 lililofanyika kwenye Hoteli ya Golden Tulip mjini Zanzibar tarehe 05
Februari 2024.
Kongamano hilo ambalo ni la tatu kufanyika ni utekelezaji wa
maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
ya kushirikisha wananchi kutoa maoni yatakayozingatiwa katika zoezi la
kurekebisha Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001.
Mwenye dhamana ya kusimamia Sera hiyo, Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba ametaja sababu za
Wizara yake kuratibu makongamano hayo ambapo alisema linalofuata litafanyika
Pemba tarehe 10 Februari 2024.
Alieleza kufanyika kwa makongamano hayo ni utekelezaji wa
misingi ya utawala bora ambayo inasisitiza umuhimu wa kushirikisha wadau katika
utungaji wa Sera za nchi, ikiwemo Sera ya Mambo ya Nje.
Alieleza pia kuwa Sera ni Tamko linalotoa mwongozo namna
nchi itakavyoshughulikia ushirikiano na uhusiano wake na dunia. Hivyo, utungaji
wa Tamko muhimu kama hilo lazima lishirikishe wadau wote.
Mhe. Makamba aliwambia washiriki wa Kongamano hilo kuwa
Tanzania ina ushawishi mkubwa duniani tofauti na nguvu zake za kiuchumi na kijeshi
kutokana na kuwa na Sera bora ya Mambo ya Nje. Hivyo, ili iendelee kuwa na
ushawishi huo duniani lazima itungwe Sera imara itakayozingatia maoni ya wadau
wote.
Aliendelea kueleza kuwa Sera ya Mambo ya Nje ina uhusiano wa
moja kwa moja na malengo ya Maendeleo ya nchi. Hivyo, mchakato wa utungaji wa
Sera ya Mambo ya Nje lazima ushirikishe wadau kwa kuwa maendeleo ni jambo
linalomgusa kila mmoja.
Alihitimisha hotuba yake kwa kutaja baadhi ya mambo
yaliyosababisha Serikali kufanya marekebisho ya Sera hiyo. Mambo hayo ni pamoja
na mabadiliko yanayotokea duniani kama mabadiliko ya tabianchi, uvumbuzi wa
teknolojia mpya, kuibuka kwa wadau wapya wa maendeleo wenye nguvu na ushawishi
na Watanzania wengi hawakuwepo wakati wa utungaji wa Sera Mpya ya Mambo ya Nje
ya Mwaka 2001.
Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wwkiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mhe. Idrisa Mustafa Kitwana: Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Ikulu Zanzibar, Bw. Salehe Juma Mussa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Balozi Stephen Mbundi, Naibu Katiibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa, Mabalozi wa Tanzania Nje ya Nchi, Mabolozi Wastaafu akiwemo Balozi Amina Salum Ali, viongozi wa Vyama vya Siasa, Asasi za Kiraia, Wakuu wa taasisi za Serikali na Sekta Binafsi, Wakuu wa Vyombo vya habari, wanazuoni na wananchi kwa ujumla.


0 Maoni