Ziara zinayofanywa na Maafisa kutoka Shirika la Hifadhi za
Taifa Tanzania (TANAPA) wanaoshiriki Maonesho ya 10 ya Biashara ya Kimataifa
Fumba - Zanzibar ya kuwatembelea Wadau wa utalii na Mawakala wa usafirishaji wa
anga (ndege) imeleta matumaini mapya yatakayochagiza ongezeko la wataii ndani
ya Hifadhi za Taifa, hasa upande wa Kusini unaopokea watalii wengi kutoka
Zanzibar na kuimarisha ushirikiano baina ya wadau hao na TANAPA.
Akiongea kwa furaha na matumaini makubwa, Mkurugenzi wa
Ndonga Adventure Bw. Abuu Bakari Abdallah alisema, "Nimefarijika sana kuja
kwenu na kufanya mazungumzo nami, nimegundua kuwa mnathamini mchango wangu wa
kuleta wageni katika Hifadhi za Taifa zilizoko Mashariki na Kusini mwa
Tanzania. Wageni wangu huridhishwa sana na huduma nzuri zinazotolewa Mikumi na
Nyerere na wamekuwa wakitoa au kuandika (comments) nzuri, niwapongeze sana kwa
kazi na huduma nzuri mnazotoa kwa watalii".
Aidha, Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa "Nimekuwa
nikipata ushirikiano mzuri kutoka TANAPA hata ninapopata tatizo hifadhini
maafisa na askari wenu huwa pamoja nasi hadi mwisho wa tatizo na kuna wakati
watakusubiri hadi wajue wewe na wageni wako mtalala wapi ndio waendelee na
majukumu yao."
Naye, Mwakilishi wa Auric Air Zanzibar - Bi. Hajra Hazaa,
aliwashuru TANAPA kwa ujio wao katika Ofisi za Auric Air zilizopo katika Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar na kuliomba Shirika hilo lenye Makao Makuu
yake jijini Arusha kuboresha miundombinu ya barabara na Viwanja vya ndege.
Afisa Mwandamizi anayeshughulikia masuala ya Utalii Hifadhi
Taifa Mikumi - Herman Baltazary, aliwahakikishia wadau hao maboresho makubwa ya
ujenzi wa barabara na Viwanja vya ndege yanayofanyika ndani ya Hifadhi za Taifa
Mikumi, Ruaha na Nyerere inayotekelezwa kupitia Mradi wa REGROW.
"Nikushauri pia kutumia Kiwanja cha Ndege cha Msolwa
ili wageni wenu waweze kulala na kupata nafasi ya kutembelea Hifadhi za Taifa
Udzungwa kwa ajili ya kupanda mlima na kujionea Maporomoko ya Sanje, Mikumi na
Ruaha kuangalia wanyama na nyika tofauti bila kuisahau Nyerere kwa ajili ya
"boat safari". Kwa kufanya hivyo wageni wenu watakuwa wamepata vionyo
na radha tofauti ya utalii," aliongeza mwandamizi huyo.
Ziara ya Maafisa kutoka TANAPA kuwatembelea wadau wa utalii ilianza takribani siku nne zilizopita na leo tarehe 16.01.2024 imendelea katika viunga na ofisi mbalimbali za wadau wa utalii na mawakala wa usafirishaji walioko Zanzibar.
Na. Jacob Kasiri- Zanzibar
0 Maoni