Wazazi wameaswa kufuatilia michezo ya watoto kwa karibu
zaidi na kuwazuia kuweka vitu mdomoni, puani pamoja na maskioni ili kuwaepusha
na madhara mbalimbali ikiwemo madhara ya kudumu na kifo.
Kauli hiyo imetolewa na Jopo la Madaktari Bingwa wa Upasuaji
wa Kifua na Moyo, Mapafu na Mfumo wa Upumuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili
ambao wameshiriki kuondoa shanga ya plastiki iliyokuwa imekwama katika pafu la
kulia la mtoto mwenye umri wa miaka mitano.
Daktari Bingwa wa Mapafu na Mfumo wa Upumuaji, Dkt. Mwanaada
Kilima amesema, shanga hiyo iliingia kwenye pafu baada ya kumpalia mtoto
alipokuwa akiichezea mdomoni takribani mwezi mmoja uliopita.
Dkt. Kilima amesema mtoto huyo alitaabika tangu wakati huo
kwa kikohozi na kupumua kwa shida huku njia mbalimbali zikitumika kujaribu
kuitoa na kugonga mwamba, ndipo wataalamu wa mapafu walipofanikiwa kuitoa bila
madhara yoyote.
“Tulitumia mpira laini wenye kamera ya video ya mapafu
(Flexible bronchoscope) na kifaa cha kukamatia (foreign body basket) na
kufanikiwa kuitoa hivyo kumwepusha na upasuaji mkubwa ambao ungesababisha ama kutoa
pafu au sehemu ya pafu,” amesema Dkt. Kilima.
Dkt. Ramadhan Hamis, Bingwa wa Upasuaji wa Kifua na Moyo ndiye aliyeoongoza jopo hilo kwa kushirikiana na Dkt. Charles Komba Bingwa wa Upasuaji Kifua pamoja na Dkt. Mwanaada Kilima Bingwa wa Mapafu na Mfumo wa Upumuaji.
0 Maoni