Zaidi ya Watanzania 400 watalii wafungua mwaka 2024 - Mikumi

 

Zaidi ya watalii 400 wa ndani wafungua mwaka 2024 katika Hifadhi ya Taifa Mikumi kufuatia kampeni kabambe iliyoendeshwa na TANAPA kupitia Hifadhi ya Taifa Mikumi ambapo watalii hao kutoka mikoa ya Dar es salaam, Morogoro na Dodoma walihamasika kutembelea Hifadhi ya Taifa Mikumi kufanya utalii wa ndani, kufunga mwaka 2023 na kufungua mwaka 2024.

Akishiriki mkesha huo wa kuupokea mwaka 2024 ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima alipongeza kazi kubwa inayofanywa na TANAPA kwa kufuata maono makubwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Niwapongeze sana TANAPA kazi mnayoifanya ni kubwa na inaonekana lakini kipekee kabisa nimpongeze Mhe. Rais kupitia filamu yake ya The Royal Tour dunia nzima sasa inatujua. Kuna msemo usemao "ukibebwa shikilia" Mhe. Rais keshamaliza kazi yake tuliobaki ni sisi na TANAPA kuendeleza jitihada hizo. Jana niliambiwa zaidi ya watalii 700 waliingia Mikumi wakitokea Zanzibar.”

Aidha, Mhe. Malima alibainisha mipango mbalimbali ya mkoa ikiwa ni pamoja na kukutana na makampuni ya utalii, waongoza watalii pamoja na wamiliki wa hoteli za kitalii ili kuangalia namna bora ya kuwezesha wageni kutumia siku zaidi katika Hifadhi ya Taifa Mikumi.

Awali, akimkaribisha Mkuu wa mkoa katika hafla hiyo ya kuupokea mwaka 2024, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Kamishna Ignas Gara alisema kuwa Hifadhi ya Taifa Mikumi imepokea idadi kubwa ya watalii kutokana na filamu ya The Royal Tour iliyoasisiwa na Rais mhe. Dkt. Samia.

“Kipekee tufikishie shukrani zetu kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani tumeshuhudia idadi kubwa ya wageni wa nje na ndani wakiongezeka, wewe mwenyewe hata sasa unajionea idadi kubwa ya watanzania waliofika na wanaoendelea kufika ili wajionee vivutio vilivyomo katika hifadhi hii, nyota njema huonekana asubuhi kiufupi tumeanza vizuri na tuko vizuri sana.” aliongeza Kamishna Gara.

Hifadhi ya Taifa Mikumi ni miongoni mwa hifadhi 21 zinazosimamiwa na TANAPA. Hifadhi hii iko mkoani Morogoro na inasifika kwa kuwa na makundi makubwa ya Nyati, tembo, Simba, swala wa aina mbalimbali, twiga na  Viboko.

Na. Edmund Salaho- TANAPA.

Chapisha Maoni

0 Maoni