Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Dkt. Batilda Salha Burian
ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA kwa jitihada za dhati za kukuza utalii
Mkoani Tabora.
Dkt. Batilda alitoa pongezi hizo alipotembelewa na Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda ofisi
kwake akiwa katika ziara ya kikazi Kanda ya Magharibi iliyokuwa na lengo la
kukagua shughuli za uhifadhi na utalii zinazofanywa na TAWA Mkoani humo.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema anatambua jitihada zinazofanywa na
TAWA katika kuboresha miundombinu ya utalii katika bustani ya Wanyamapori
Mkoani humo ijulikanayo kama Tabora ZOO na kuishauri Mamlaka hiyo kuangalia
uwezekano kuongeza miundombinu katika bustani hiyo kwa ajili ya kuongeza
mapato.
Vilevile, alishauri kuongeza mazao mbalimbali ya wanyamapori
kama vile sumu ya nyoka ambapo alisema kuwa inahitaji utafiti zaidi.
Pia Dkt. Batilda alisema ili kuendelea kuchagiza shughuli za
utalii Mkoani humo, TAWA ione namna bora ya kushirikiana na sekta binafsi
katika kuimarisha uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali yenye vivutio vya utalii
ikiwemo bustani ya wanyamapori ya Tabora.
Aidha, aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa TAWA ili
kuhakikisha shughuli za Uhifadhi na Utalii zinazofanywa na taasisi hiyo
zinazidi kuimarika.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi
Nyanda alimshukuru Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora kwa ushirikiano na mshikamano
anaoutoa kwa taasisi yake anayoiongoza katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya
kiuhifadhi na utalii Mkoani humo
Ziara ya Kamishna Mabula katika Kanda ya Ziwa, Kati na Magharibi ililenga
kukagua shughuli mbalimbali za uhifadhi na utalii zinazofanywa na TAWA katika
Kanda hizo ikiwa ni pamoja na kukagua miradi mbalimbali kama vile ujenzi wa
karakana ya kutengenezea magari na mitambo Wilayani Manyoni.
Pia kuzindua jengo la ofisi ya Pori la Akiba Moyowosi Wilayani Kibondo na kutembelea familia za ndugu walioathiriwa na wanyamapori aina ya mamba na kuwapa pole katika vijiji vya Kasahunga na Mayolo wilayani Bunda
Na. Beatus Maganja- Tabora
0 Maoni