Mzazi aagiza akamatwe kijana wake aliyejaribu kumzuia asiondoke ndani ya hifadhi

 

Katika hali isiyo ya kawaida bwana Kashiro Ndete amefanya maamuzi magumu na kutaka kijana wake akamatwe na jeshi la polisi baada ya kijana huyo kutaka kumzuia baba yake asihame kwa hiyari katika eneo la hifadhi na kuleta vurugu wakati mzazi huyu na familia yake wakijiandaa kuondoka katika eneo hilo.

Mzee Kashiro Ndete ambaye pia ni kiongozi wa Mila (Laigwanan) na miongoni mwa wananchi 515 waliohamia Msomera ijumaa ya wiki hii amesema kuwa alifanya uamuzi wa kuhama ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha maisha ya wananchi wanaokwenda kuishi nje ya hifadhi.

Alisema kuwa kijana wake huyo aliyemtaja kwa jina la Leepalai anamtuhumu kwa kutaka kumzuia yeye na familia yake na Watoto wake wengine wasiondoke wabaki ndani ya hifadhi bila kuwa na sababu za msingi za kufanya hivyo.

“Vijana wa siku hizi hawana adabu,yeye ni mwanangu wa kumzaa na hana boma, nyumba ni mali yangu na nimeamua kuhama kwa hiyari hawezi kutaka kunifanyia fujo halafu nikamwacha hivi hivi, lazima vyombo vya dola vichukue mkondo wake,” alisema Kashiro.

Katika utekelezaji wa zoezi la kuhamisha watu kwa hiyari kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kumekuwa na changamoto ya baadhi ya watu kuwashawishi wananchi wanaojiandikisha kwa hiari yao wenyewe wasihame na hivyo kutumia mbinu mbalimbali ili kuwazuia wale waliokubali kuondoka.

Chapisha Maoni

0 Maoni