Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kusini - TANAPA, Steria Ndaga
amesema uwepo wa Soko la Kimkakati la Utalii Zanzibar limechangia kwa kiasi
kikubwa ongezeko la watalii katika Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) hususan,
Hifadhi za Taifa Kanda ya Kusini na Mashariki ukilinganisha na miaka ya nyuma
ambapo wageni wengi walikuwa wakitoka ukanda wa Kaskazini. Kamanda huyo
ameyasema hayo leo tarehe 19.01.2024 kisiwani Zanzibar.
Akiwa katika Viwanja vya Maonesho ya 10 ya Biashara ya
Kimataifa Fumba - Zanzibar, Kamanda Ndaga alisema, "Maonesho haya ni sehemu ya mkakati wetu
na wadau wa utalii kuhakikisha vifurushi vinavyouzwa katika Hifadhi za Taifa
vinakuwa na idadi kubwa ya watalii wanaotumia muda mwingi hifadhini ili kuliongezea
taifa mapato."
Itakumbukwa mwishoni mwa mwezi Agosti, 2023 Kamisheni ya
Utalii Zanzibar (ZCT) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) walisaini mkataba wa
ushirikiano wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko Tanzania bara na Visiwani
ili kuongeza idadi kubwa zaidi ya watalii itakayofikia adhma ya watalii milioni
5 ifikapo Juni, 2026.
Naye, Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Mashariki - TANAPA,
Massana Mwishawa alisema, "Lengo la
kufika Zanzibar kwenye maonesho haya ni kuwahamasisha wazawa na wageni
kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana ndani ya Hifadhi za Taifa
Tanzania".
Aidha, Kamanda Mwishawa aliongeza kuwa uwekezaji unaotakiwa
ndani ya hifadhi hizo ni pamoja na ujenzi wa malazi ya muda na ya kudumu ili
kuongeza huduma za malazi kwa wageni ndani ya hifadhi. Hata hivyo aliendelea
kufafanua kuwa kwa Kanda za Kusini na Mashariki kuna maeneo ya uwekezaji zaidi
ya 60 huku Hifadhi ya Taifa Nyerere pekee ikiwa na idadi ya maeneo ya uwekezaji
38.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Abel Mtui alisema,
"Ongezeko la miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege vimeimarishwa
ili kuwezesha wageni kufika hifadhini bila adha yoyote. Kupitia Mradi wa Serikali (REGROW) kuna takribani
viwanja vinne vya ndege vyenye uwezo wa kutua ndege zenye uwezo wa kubeba
abiria 50.
Vilevile, Kamishna Abel aliongeza kuwa kukamilika kwa
viwanja vya ndege hivyo vitaongeza ufanisi na kuunganisha safari za wageni
kutoka hifadhi moja kwenda nyingine. Hifadhi zitakazofaidika safari hizo ni
Hifadhi za Taifa Mikumi, Ruaha, Nyerere, Saadan, Katavi, Udzungwa na Kitulo.
Sekta ya utalii kwa upande wa Tanzania bara inachangia kiasi cha asilimia 17 katika pato la Taifa, wakati kwa upande wa Zanzibar inachagia asilimia 30. Kwa mantiki hiyo uboreshaji wa miundombinu hiyo itaongeza idadi ya watalii nchini.
Na. Jacob Kasiri- Zanzibar
0 Maoni