Jumla ya Km.186 za barabara zimekamilika kuchongwa na
kilometa 24 zimewekewa changarawe kati
ya Km. 986 za mtandao wa barabara katika Kijiji cha Msomera, wilayani Handeni.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Wilaya ya Handeni Mhandisi
Judica Makyao wakati ya ziara ya
Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff katika kijiji cha Msomera.
Ameeleza kuwa kazi ya kufungua barabara zinaendelea kwa
awamu ambapo Kilometa hizo zinajumuisha
maeneo ya mashamba, huduma za kijamii pamoja na makazi yaliyojengwa
katika eneo la mradi huo.
“Kazi hizi zimekua zikifanyika kwa awamu na kwa sasa wakandarasi wapo kazini
wanaendelea na ufunguzi na uchongaji wa barabara pamoja na ujenzi wa Makalavati 10 kwenye eneo
la mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi na maeneo mengine”. Alisema Mhandisi
Makyao.
Katika ziara hiyo Mtendaji Mkuu huyo Mhandisi Victor Seff
alisema TARURA itaendelea kutoa ushirikiano na kuhakikisha ujenzi wa barabara
katika kijiji hicho unakuwa wa viwango vilivyokusudiwa ili kufikia adhima na
malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan.
Aidha, Mhandisi Seff
alimpongeza Msimamizi wa ujenzi wa mradi huo Kanali Sadick Mihayo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya ujenzi wa
makazi ya wafugaji wanaohamia kijijini Msomera.
Naye, Msimamizi wa Ujenzi wa Mradi wa Makazi ya Wafugaji
Kanali Sadick Mihayo amempongeza
Mhandisi Seff kwa ushirikiano mkubwa unaotolewa na watendaji wa TARURA-wilaya
ya Handeni na kumpongeza Meneja wa TARURA-Wilaya ya Handeni Mhandisi Judica
Makyao kwa kujitoa kwake kikamilifu ili kuhakikisha barabara zinafunguliwa na
kupitika katika eneo la mradi.
Kanali Mihayo alieleza eneo la mradi linahusisha Halmashauri tatu za Wilaya za Handeni, Kilindi na Simanjiro
na kuwa utekelezaji rasmi wa ujenzi wa
nyumba za Makazi umeanzia katika eneo la Msomera, Wilaya ya Handeni na kwa sasa
takribani barabara zote muhimu zimefunguliwa na TARURA.
Kanali Mihayo alisema kwa awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba utakaofanyika katika Wilaya ya Kilindi na Simanjirio kwa sasa wataamu wa kupanga matumizi ya ardhi “Surveyor” wanaendelea na zoezi la kuzitambua barabara katika eneo la Kilindi na Simanjiro ili ziweze kufunguliwa na kuendelea na ujenzi.
0 Maoni