MWENDELEZO WA TAARIFA KUHUSU KUSAMBAA KWA PICHA JONGEFU (VIDEO CLIP) INAYOONYESHA MWINDAJI AKIWA NA MAMBA ALIYEWINDWA
Itakumbukwa kuwa tarehe 27/12/2023, Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWA) ilitoa taarifa ya awali kwa umma kuhusu suala hili
na kuahidi kufanya uchunguzi zaidi.
TAWA inapenda kuufahamisha umma kuwa uchunguzi kuhusu suala
hili umekamilika. Hivyo, taarifa ifuatayo inatoa ufafanuzi kuhusu uwindaji wa
mamba husika na dhana nzima ya uwindaji nchini na duniani.
Shughuli za uwindaii ikiwemo wa mamba nchini zipo kisheria
zikisimamiwa na Sheria za ndani na za kimataifa kupitia Mkataba wa Kimataifa wa
biashara ya wanyamapori na mimea iliyohatarini kutoweka (Convention on
International Trade in Endangered Species of Wild Fauna and Flora - CITES).
Kwa mujibu wa taratibu za mkataba wa kimataifa wa CITES,
Tanzania imeruhusiwa kuwinda mamba wasiozidi 1,600 kwa mwaka. Mpaka sasa jumla
ya mamba 39 tu kati ya 1,600 wamewindwa kutoka kwenye mgawo (quota) wa Taifa wa
mwaka 2023.
Mamba anayeonekana kwenye picha jongefu (video clip)
iliyosambaa aliwindwa katika kitalu cha Lake Rukwa GR kwa kibali halali namba
MP-0001792 kilichoanza tarehe 12/08/2023 hadi 09/09/2023.
Mamba huyo alikuwa na urefu wa futi 16.2 sawa na sentimita
493.8 ikiwa ni juu ya kiwango cha chini cha urefu wa sentimita 300 unaohitajika
kwa mujibu wa Sheria. Aidha, kwa mujibu wa takwimu za taasisi ya Marekani
(Safari Club International - SCI), mamba mrefu zaidi duniani aliwindwa nchini
Ethiopia mwaka 2005 (futi 18.7 sawa na sentimita 561).
Vilevile, kumbukumbu zinaonesha, uwindaji huu ulisimamiwa na
askari kutoka TAWA na mwindaji bingwa kutoka kwenye kampuni iliyopewa kibali
kwa mujibu wa Sheria. Aidha, ada na tozo
zote zinazohusiana na uwindaji wa mamba zililipwa kwa kuzingatia Sheria na
Kanuni zinazosimamia uwindaji hapa nchini.
Wakati uwindaji ukifanyika askari anayesimamia uwindaji
uhakikisha uwindaji unafanyika kwa kuzingatia Sheria na kulinda usalama wa
wageni wawindaji na watu walioambatana nao. Hivyo taratibu zote hizi za
kisheria zilizingatiwa na hakuna utaratibu uliokiukwa.
Kwa taarifa hii, umma unahakikishiwa kuwa uwindaji wa
wanyamapori nchini unazingatia Sheria na taratibu za ndani ya nchi na zile za
kimataifa na Mamlaka inawatoa hofu kuwa taratibu hizi zinasimamiwa ipasavyo na
pale panapotokea ukiukwaji hatua stahiki huchukuliwa kwa mujibu wa Sheria.
Mamlaka inawashukuru watanzania wote waliopaza sauti zao
wakionesha utayari wa kulinda rasilimali zetu na kutaka kujiridhisha kuhusu
uhalali wa uwindaji husika.
Imetolewa na:
Beatus Maganja
AFISA HABARI
KITENGO CHA UHUSIANO KWA UMMA - TAWA
0 Maoni