Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amesema kuwa, uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu
nchini, usiwe kigezo cha kugawa wananchi bali watu wote waungane, wapendane na
wathaminiane ili kuendelea kudumisha amani iliyopo.
Mhe. Dkt. Biteko amesema hayo jana wakati alipojumuika na wananchi wa Bukombe katika sherehe za kuukaribisha mwaka
2024 nyumbani kwake kitongoji cha Bulangwa, wilayani Bukombe mkoani Geita
ambapo ametoa pia salam za mwaka mpya.
"Mwaka huu utakuwa mwaka wa uchaguzi wa Serikali za
Mitaa, kamwe uchaguzi huu usitugawe kwa misingi ya vyama vya siasa lakini
utuunganishe zaidi, watu wote tunapaswa tupendane, tuthaminiane na
tushirikiane, tunazo tofauti nyingi
ikiwemo za makabila, dini na vyama vya siasa lakini kamwe visitugawanye,
tuungane wote na tushikamane," amesema
Dkt. Biteko.
Kuhusu Salam za Rais, Dkt. Samia za Mwaka 2024 alizozitoa
kwa watanzania, Dkt. Biteko amesema, Sekta ya Nishati itaiishi kauli ya Rais ya
kuwa, mwaka 2024 utakuwa ni mwaka wa vitendo na si maneno na kwamba watafanyia
kazi maelekezo yake kwa nguvu zote na ubunifu ili wananchi wapate huduma bora.
Dkt. Biteko ameshukuru wananchi wa Bukombe kwa ushirikiano
wanaompa katika utekelezaji wa majukumu yake akieleza kwamba watu wa Bukombe wamekuwa si watu wa
kunung'unika bali kuboresha pale wanapoona kuna upungufu.
Akitoa salam salam za mwaka mpya 2024, Dkt. Biteko ametaka
wananchi kupendana, kuthaminiana na kushirikiana na kila mtu aazimie kumfanya mtu mmoja awe na
furaha na kusameheana.
Sherehe za kukaribisha mwaka 2024 wilayani Bukombe
zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita,
Martine Shigella, Wabunge wa Mkoa wa
Geita, Madiwani wa Kata mbalimbali wilayani Bukombe na viongozi wa Vijiji.
Huu umekuwa ni utamaduni ambao Dkt. Doto Biteko amekuwa
akiufanya kutoka mwaka 2016 wa kujumuika na wananchi katika kukaribisha mwaka
mpya.
Mgeni maalum katika sherehe hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita,
Martine Shigella amempongeza Dkt. Biteko kwa utamaduni huo, ambao haubagui
dini, kabila, itikadi za kisiasa au hadhi ya mtu.
Amesema utaratibu huo umewezesha wananchi kujumuika pamoja, kufurahi, kutafakari yale waliyofanikiwa na yaliyoshindwa kufanikiwa, kuweka jitihada katika mwaka 2024 na kuweka mikakati ya nini kifanyike katika mwaka huuili Jimbo la Bukombe liweze kusonga mbele.
0 Maoni