Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya Yakobi iliyopo katika
Kijiji cha Limage, Halmashauri ya Mji Njombe mkoani Njombe, Editor John amesema
kuwa kutokana na Serikali kupeleka fedha kwa ajili ya kuongeza mabweni, udahili
wa wanafunzi umeongezeka kutoka wanafunzi 105 hadi 433.
Ameyazungumza hayo hivi karibuni wakati akihojiwa na Maafisa
Habari kutoka Idara ya Habari (Maelezo) ambapo amesema kuwa, jumla ya shilingi
milioni 543 zilipelekwa na Serikali kwa ajili ya upanuzi wa miundombinu ya
elimu kwa ajili ya kidato cha tano na sita ambapo fedha hizo zimeweza kujenga
mabweni matatu ya watoto wa kike, madarasa matano pamoja na matundu 14 ya vyoo.
“Tulifanikiwa kutekeleza ujenzi wa mabweni matatu ambayo
yamekamilika na wanafunzi wanaishi, madarasa matatu, ofisi moja, matundu 16
badala ya 14 pamoja na samani za ndani ya mabweni ambapo ilitakiwa kununua
vitanda vya deka 120 lakini kupitia matumizi mazuri ya fedha hizo, vilinunuliwa
vitanda vya deka 180 na badala ya kununua viti 200 na meza 200, imewezekana
kununua viti 380 na meza 380, alisema
bi. Editor.
Bi. Editor ameongeza kuwa, mnamo mwezi Agosti, 2023 Serikali
ilileta tena jumla ya shilingi milioni 130 kwa ajili ya ujenzi wa bweni lingine
la wasichana ambalo linakaribia kukamilika. Aidha, ameishukuru Serikali kwa
ujio wa fedha hizo kwani sio mara ya kwanza kuwakumbuka, hata kipindi cha
kwanza cha kuanzisha kidato cha tano na cha sita, ilipeleka jumla ya shilingi
milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa bweni ambalo kwa kiasi kikubwa limewasaidia
wanafunzi kusoma katika mazingira bora na wote kufaulu kwa daraja la kwanza
hadi la tatu.
Kwa upande wake mwanafunzi, Amokile Sanga amesema kuwa,
mabweni hayo yamekuwa msaada mkubwa kwani wanalala vizuri bila kubanana na ni
mabweni bora kwa kuwa yamejengwa kisasa, ameeleza kuwa taaluma bora huwa
inaendana na miundombinu bora hivyo kuongezeka kwa mabweni hayo kumewasaidia
kuwa na taaluma bora.
"Uwepo wa mabweni haya umesaidia watoto wa kike kuwa na
mazingira bora ya kupata elimu kwani wasichana wengi wanaosoma shule za kutwa
hukutana na vikwazo vingi njiani ambavyo hukatisha ndoto zao za kupata
elimu," alisema Amokile.
Naye mwanafunzi Nancy Abraham amemshukuru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani pamoja na ujenzi wa
mabweni uliosababisha udahili wa wanafunzi kuongezeka, bado alitoa fedha kwa
ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu na madarasa matano yanayoendana na wingi wa
wanafunzi hao.
Akizungumza kwa ujumla, Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya
Mji Njombe, Mwalimu Prochesius Mguli amesema kuwa Serikali imeleta fedha nyingi
kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu ambapo kwa mwaka 2022/23, Halmashauri ya
Mji Njombe ilitekeleza baadhi ya miradi ikiwemo ujenzi wa nyumba za Walimu (2
in 1) katika Shule ya Sekondari Lunyanywi ambapo zililetwa jumla ya shilingi
milioni 100 na tayari ujenzi wake umeshakamilika, pia kupitia mradi wa SEQUIP,
Serikali imeleta shilingi milioni 583.1 ambayo imetumika kujenga shule ambayo
itaanza rasmi mwaka 2024.
Na. Jacquiline Mrisho - Maelezo
0 Maoni