Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi Maliasili na Utalii
imeipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kufanya Kazi
kubwa na nzuri ya Maboresho ya Mfumo
Unganishi wa Usimamizi wa Sekta ya Ardhi inayofanywa na timu ya wataalamu
mkoani Arusha.
Akizungumza mara baada ya hitimisho la wasilisho la kazi ya
uboreshaji mfumo huo, Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Timotheo Mzava ameipongeza
Wizara ya Ardhi kwa kazi kubwa na nzuri na kueleza kuwa kazi hiyo inakwenda
kuacha alama kwa Mhe Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha uongozi
kwa kuiacha sekta ya ardhi katika mifumo bora.
"Nichukue fursa hii kumpongeza Mhe Rais kwa kazi hii nzuri, kama kamati wameridhishwa
na kazi na hongereni sana na mfumo huu uende ukawe bora na kutoa huduma kwa
watanzania" alisema Mhe Mzava.
Baadhi ya wabunge wamesema mfumo huo siyo tu utarahisisha na
kuharakisha huduma za sekta ya ardhi bali utajibu maswali mengi yakiwemo ya
kijamii.
"Niipongeze wizara ya ardhi kwa kufanyia kazi mfumo
utakaojibu maswali mengi ya kijamii na ningetamani mfumo huu ungejibu maswali
na changamoto za kiuchumi" alisema Mhe. Lucy Mayenga mbunge wa viti
Maalum.
Mbunge Makete mkoani Njombe Festo Sanga aliipongeza Wizara
kwa kuboresha mfumo na kueleza kuwa uboreshaji huo umechelewa ingawa uko katika
hatua nzuri. Hata hivyo, mbunge huyo wa Makete alitaka kufahamu utayari wa
wizara ya Ardhi katika kutumia mfumo hususan kwenye eneo la usalama wa mifumo.
Aidha, Mbunge wa jimbo la Tabora Mjini Emanuel Adamson mbali
na kuipongeza wizara kwa kuboresha mfumo
alitaka kufahamu uimara wa utekelezaji mfumo huo kwa kuwa kumekuwa na
mifumo mingi lakini wakati wa utekekezaji kumekuwa na changamoto ikiwemo
kuekezwa mtandao uko chini.
Mfumo huo unganishi wa usimamizi wa sekta ya ardhi unatarajiwa kuanza katika mikoa mitano ya Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Tanga na utarahisisha na kuharakisha upatikanaji huduma za sekta ya ardhi kwa kuwa wananchi watakuwa wakipata huduma kwa njia ya mtandao.
Na. Munir Shemweta- WANMM ARUSHA
0 Maoni