WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Maji Jumaa
Aweso kufika katika ofisi za wakala wa Maji na usafi Mazingira Vijijini Mkoa wa
Lindi (RUWASA) na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Lindi (LUWASA)
kufuatilia mapungufu yaliyopo ikiwemo kutotumika kwa gari la uchimbaji visima
lililotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu Juni, 2023 ili
kuwezesha uchimbaji wa visima vya maji.
“Hii wizara ina Waziri makini sana, mnafanya vitu kwa
ufichouficho, sasa Waziri aje hapa, mnamuona anavyohangaika Waziri wenu, vitu
vidogo vidogo hivi mpaka waziri aje na ninyi mpo, kwanini mpo hapa,” Waziri
Mkuu alisisitiza na kuongeza kuwa anahitaji taarifa ya kwa nini mashine hiyo
tangu imefika haijachimba kisima hata kimoja.
Ametoa agizo hilo leo Jumatatu, Januari 8, 2024, baada ya
kufanya ziara katika ofisi za RUWASA zilizopo Manispaa ya Lindi na kushuhudia
mtambo wa kuchimba visima ukiwa umeegeshwa na hakuna kisima kilichochimbwa
tangu ulipotolewa mwaka jana huku katika mikoa mingine iliyopewa mtambo kama
huo visima vinachimbwa kama ilivyokusudiwa.
Waziri Mkuu amehoji “Ni kwanini mtambo huu haujaanza kufanya
kazi kwa kipindi cha miezi sita ikiwa katika mikoa mingine imeshaanza kufanya
hivyo. Mwezi wa sita hadi leo hamjachimba hata kisima kimoja na mnasema kuna
matope haiwezekani. Mheshimiwa Rais ameleta mtambo wananchi wameona gari
limefika mnataka visima visichimbwe?”.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu alihoji sababu ya kutotumika kwa
pikipiki zilizonunuliwa na RUWASA Mkoa wa Lindi tangu mwaka 2021 kwa ajili ya
kuzigawa kwa jumuiya za watumia maji kwa madai kuwa bado hazijapata usajili.
“Huu ni uzembe haiwezekani fedha za wananchi zinapotea nyie mpo tu. Hizi
pikipiki zimeanza kuharibika.”
Akizungumzia kuhusu pikipiki hizo Afisa Manunuzi wa Wakala
wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Mkoa wa Lindi (RUWASA) Bw. Kenedy Mbagwa
alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakifuatilia suala la vibali vya kutumia
pikipiki hizo kutoka makao Makuu ya RUWASA bila ya mafanikio, ambapo Waziri
Mkuu baada ya kupata maelezo hayo amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kupambana na
Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Lindi afuatilie suala hilo.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amechukizwa na hali ya mazingira
ya ofisi ya LUWASA ambayo haiendani na ofisi za umma kwani ni machafu na yana
vichaka vingi. “Hapa ndio ofisini, kwa hiyo hapa tupo kazini,” alihoji wakati
alipokuwa akikagua maeneo hayo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Maji
na Msajili wa Hazina wafanye tathmini ya kina kuangalia utendaji kazi wa Wakala
wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) ambayo ipo ndani ya Ruwasa
kuona kama ipo haja ya taasisi hiyo kuendelea kujitegemea. “Hamuwezi kuwa na
agency mbili, zinazofanya kazi moja kwenye taasisi moja.”
Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA mkoa wa Lindi, Mhandisi Muhibu Lubasa alisema mkoa umejipanga kuanza kuchimba visima katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo kwa kutumia mtambo huo uliotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuanzia mwezi Februari mwaka huu.
0 Maoni