MAADHIMISHO ya kumbukumbu ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar
yaliyofanyika Januari 12, 1964 ni muhimu sana kwani yanaukumbusha umma wa
Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla kuhusu uzalendo uliofanywa na waasisi wa
Taifa hili katika kuwatetea wananchi wanyonge.
Ni ukweli usiopingika kuwa historia inachangia kujaza moyo
wa uzalendo kwa wananchi kwani huwafanya waone thamani ya kila hatua ya
maendeleo Kwa maneno mengine historia ina mchango mkubwa katika kuongeza ari
kwa wananchi kuitumikia nchi yao na kujiletea maendeleo pamoja na kuthamini
kazi kubwa iliyofanywa na waliotangulia.
“Ninafahamu wengi wetu hasa makundi ya vijana hatukuwepo
wakati Mapinduzi ya Mwaka 1964 yanafanyika licha ya kuwa ndio tumekuwa
wafaidika wakubwa wa Mapinduzi yale.
Hivyo basi, sisi sote hatuna budi kuyaenzi Mapinduzi hayo matukufu na
kuendelea kuyatetea na kuyalinda kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vile
vijavyo.”
Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Jumatano,
Januari 10, baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Skuli ya Muungano
iliyopo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar. Skuli hiyo ambayo
itakuwa na madarasa 41 itagharimu shilingi bilioni 6.1 mpaka kukamilika kwake.
Uwekaji huo wa jiwe la msingi ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka
60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Alisema maadhimisho hayo ni fursa kwa vijana kufahamu
historia ya nchi yao. “Sote tunafahamu kuwa Mapinduzi yanafundishwa katika somo
la historia, lakini kupitia mikusanyiko kama hii na mwendelezo wa mijadala
inayofanyika katika kipindi kama hiki inaongeza ufahamu zaidi kwa jamii yote.
Lakini pia ni ishara ya kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar na kuthamini jitihada
iliyofanywa na wazee wetu katika kutuletea uhuru.”
Mheshimiwa Majaliwa alisema kupitia Mapinduzi ya Mwaka 1964,
Zanzibar imeweza kupiga hatua kubwa katika kuwaletea wananchi wote maendeleo
bila ya ubaguzi wa aina yoyote kwani kabla ya Mapinduzi hakukuwa na fursa sawa
katika upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo huduma ya elimu.
Alisema awali shule zilikuwa chache na hivyo elimu ilikuwa
ikitolewa kwa misingi ya kibaguzi kutegemea na matabaka na jamii kubwa ya
Wazanzibar na watoto kutoka familia za kinyonge zilikosa fursa ya kupata elimu,
kwa wale wachache waliobahatika basi walisoma katika shule zenye hadhi za chini
kabisa. “Kwa msingi huo sina shaka mtakubaliana nami kuwa ilikuwa ni lazima
mapinduzi yafanywe ili kuleta usawa kwa Wazanzibar wote.”
”…Kama mnavyofahamu, sababu kubwa ya kufanyika Mapinduzi
ilikuwa ni kuchoshwa na hali ya ubaguzi mkubwa wa utawala wa kikoloni. Na huu
ndio msukumo uliosababisha Mwezi Januari 1964, Wazanzibar walishikamana na
kuamua kwa pamoja kuuondoa na kujiweka huru na udhalilishaji na madhila
waliokuwa wakifanyiwa. Wazanzibar walipambana kumuondoa mkoloni kwa kufanya
Mapinduzi ambayo leo hii tunajivunia kutimiza miaka 60 kwa kupiga hatua
mbalimbali za Maendeleo.”
Aliongeza kwa kusema kuwa, “Uhuru tulionao sisi sote katika wakati huu umetokana na ndugu zetu waliojitolea, wakiongozwa na Jemedari wa Mapinduzi Hayati Mzee Abeid Amani Karume, Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi. Hivyo basi, sote hatuna budi kuijua vizuri historia hii, kuiheshimu na kutoisahau katika maisha yetu kwa kurithisha vizazi na vizazi, kuilinda na kutorudi nyuma.”
Mheshimiwa Majaliwa alisema maadhimisho hayo yanawakumbusha
mwisho wa utawala wa kibeberu kwani Mapinduzi ya mwaka 1964 yalifanywa ili
kuuondoa utawala wa kikoloni na kujitawala wenyewe wakiwa huru katika kujiletea
maendeleo yao ya kijamii, kiuchumi na kisiasa hasa katika ulimwengu huu wa
karne ya 21 ya sayansi na teknolojia.
Mapinduzi ya 1964 yamefungua fursa za huduma mbalimbali za
maendeleo ya kijamii na kiuchumi Zanzibar zikiwemo elimu. Serikali huru ya
Zanzibar katika kuendeleza misingi ya mapinduzi imeendelea kufanya mageuzi
makubwa katika utoaji wa huduma mbalimbali za jamii kwa wananchi wake ili
wafaidi matunda ya uhuru wao.
MAFANIKIO KATIKA SEKTA YA ELIMU
Waziri Mkuu alisema historia ya mageuzi katika sekta ya
elimu ilianza tarehe 23 Septemba 1964, ambapo Serikali ya Mapinduzi
iliyoongozwa na Hayati Mzee Abeid Aman Karume, Mwenyezi Mungu amrehemu,
ilitangaza elimu bure kwa wananchi wote bila kujali rangi, kabila, dini, eneo
wanalotoka au hata jinsia., mpango wa elimu bure umeendelea kudumishwa katika
awamu zote za uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi leo
tunapoadhimisha miaka 60 sasa tangu kufanyika Mapinduzi hayo.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa alitumia fursa hiyo kueleza
baadhi ya mafanikio yaliyopatikana upande wa sekta ya elimu katika kipindi cha
miaka 60 ya Mapinduzi kuwa pamoja na uwepo
wa vyuo saba vinavyotoa masomo ya ngazi ya elimu ya juu ambapo kabla ya
Mapinduzi hakukuwa na Chuo Kikuu hata kimoja.
Alisema vijana mbalimbali wanaomaliza masomo yao ya
sekondari sasa wanapata fursa ya kujiunga na masomo ya vyuo vikuu ndani na nje
ya Tanzania, ambapo katika kipindi hiki, idadi ya wanafunzi waliosajiliwa
katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) pekee imefikia wanafunzi 7,250
mwaka huu wa 2023 kutoka wanafunzi 53 mwaka 2000 kilipoanzishwa.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali imefanikisha
kuanzisha Tawi la Chuo cha Teknolojia, Institute of Technology Madrsa (IITM)
cha India ambacho ndio chuo cha kwanza kwa ubora nchini India. “Uwepo wa chuo
hiki kunaifanya Zanzibar kuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kuwa na Tawi la chuo
hicho na hivyo kutoa fursa kubwa kuitangaza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla
Kimataifa.”
Alisema uanzishwaji wa chuo hiko ni katika hatua ya
utekelezaji wa Dira ya Maendelo ya Zanzibar ya 2050 inayoelekeza kuimarisha
ujuzi na utaalamu kwa wananchi katika kufikia uchumi na jamii ilio bora na chuo
hicho kitatoa wataalamu waliobobea kwenye masuala ya teknolojia na hivyo kuwa
chachu ya utatuzi wa changamoto zinazolikabili Taifa katika sekta mbalimbali
kama vile nishati, kilimo, afya, elimu na viwanda.
“Kama mlivyosikia hapo awali, fursa za upatikanaji wa elimu
zilikuwa chache katika ngazi zote lakini kutokana na jitihada kubwa
zinazondelea kufanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mageuzi makubwa
yamefanyika katika kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa
kuongeza miundombinu ya elimu, ambapo sasa Serikali imeanza utekelezaji wa
mradi wa ujenzi wa vyuo vitano vya kisasa vya mafunzo ya Amali kote nchini.”
Alisema ujenzi wa vyuo hivyo utakamilisha shabaha ya Serikali kuwa na Chuo cha Amali kikubwa na cha kisasa katika kila wilaya kwa lengo la kuhakikisha vijana wanapata ujuzi na utaalamu utakaowasaidia kukabiliana na ushindani wa soko la ajira ndani na nje ya nchi hasa katika fani za Uchumi wa Buluu. Aidha, kupitia mradi huo, Serikali itajenga na kukipatia vifaa chuo cha ubaharia na kutanua Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ili kuongeza fani mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho zikiwemo mafuta na gesi.
“Pia, Serikali inajenga ofisi za elimu za wilaya na
kuzipatia vifaa ambazo mbili tayari zimeshafunguliwa katika sherehe hizi
zinazoendelea za maadhimisho ya kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi. Ujenzi wa ofisi
hizi utaimarisha ufuatiliaji na usimamizi katika utoaji na upatikanaji wa elimu
bora. Kuziunganisha Skuli zote na mkonga wa taifa wa mawasiliano ili kuimarisha
matumizi ya teknolojia katika kufundishia na kujifunzia.”
MAFANIKIO KATIKA SEKTA YA AFYA
Waziri Mkuu alisema Mheshimiwa Rais Dkt Mwinyi amedhamiria
kuimarisha miundombinu ya sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata
huduma katika mazingira bora na kwa viwango vinavyokubalika ikiwa ni pamoja na
kuendelea kuweka mifumo imara ikiwemo mfumo wa rufaa utakaozingatia huduma bora
zinazotolewa kwa wakati.
Alisema miradi ya ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya
inatekelezwa ili kusogeza huduma bora karibu na wananchi, kupunguza msongamano na kufanya utoaji wa
huduma za afya uwe rafiki kwa watoa huduma na kwa wananchi na kwamba ujenzi wa vituo
vya kisasa vya kutolea huduma za afya utapunguza gharama kutokana na ukweli
kwamba, kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kugharamia
matibabu ya wananchi nje ya nchi.
“Serikali imeanza na itaendelea kuimarisha miundombinu ya
kutolea huduma za afya ili madaktari bingwa na bobezi wazalendo na wale wa
kigeni waweze kuwa na mazingira rafiki ya kutoa huduma za kibingwa na kibobezi
katika hospitali zetu za kisasa zilizopo hapa nchini.”
Waziri Mkuu alisema kutokana na jitihada hizo, Serikali
imeshajenga hospitali 10 za wilaya katika wilaya za Unguja na Pemba, na kila
hospitali ina vifaa tiba kamili na magari ya kisasa ya kubebea wagonjwa kwa
ajili ya kutoa tiba stahiki za dharura na rufaa. Hospitali hizo zote ni nzuri na zina huduma zote
za kisasa kama lilivyo jengo hili la Hospitali ya Wilaya ya Kaskazini B.
Aliyasema hayo wakati akifungua Hospitali ya wilaya ya Kaskazini B Pangatupu
iliyopo mkoa wa Kaskazini Unguja.
“Mradi huu wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kaskazini B
ni matokeo ya mipango thabiti na utekelezaji wa ahadi ya Serikali yetu Tukufu
zinazokwenda sambamba na utekelezaji wa mikakati ya Mapinduzi matukufu ya mwaka
1964. Serikali iliahidi itatekeleza na leo tumefungua hospitali hii mpya ambayo
ina hadhi ya wilaya na itatoa huduma za afya kwa mfumo wa kidijitali.”
PONGEZI KWA RAIS DKT. MWINYI
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo
kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuyaendeleza na
kutekeleza malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa
vitendo.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi ni kiongozi mwenye busara,
hekima na mchapakazi mwenye kuwatumikia wananchi wake kwa kuwaletea maendeleo
wanayoyataka kwa kasi kubwa. Kila mmoja wenu ni shahidi wa mabadiliko makubwa ya
kimaendeleo yaliyofanyika Zanzibar katika kipindi kifupi.
Mbali ya hayo Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi ameendeleza umoja,
mshikamano, amani na utulivu Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ambayo imekuwa
kichocheo katika kutekeleza shughuli mbalimbali za kuwaletea wananchi
Maendeleo. Mwenyezi Mungu amzidishie afya njema hekima na busara katika
kuwatumikia zaidi wananchi. Haya ndio malengo hasa ya mapinduzi.”
Naye, Waziri wa Afya, Nassoro Ahmed Mazrui alisema takwimu
zinaonesha Zanzibar kuna mapinduzi makubwa ya huduma za afya katika sekta ya
umma kwani wametoka kuwa na vitanda 1,445 vya kulaza wagonjwa na sasa vipo
takribani vitanda 2,645 vya kulaza wagonjwa katika hospitali za Unguja na
Pemba.
Alisema awali kulikuwa na ICU moja tu ya Hospitali ya Mnazimmoja,
yenye vitanda vinane na sasa hivi kuna jumla ya ICU 14 na vitanda 80 vya ICU
ikiwa ni pamoja na vitanda sita vya ICU vilivyokuwemo ndani hospitali ya wilaya
ya Magharibi A. Pia kulikuwa na vyumba vya upasuaji 11 na kati yake viwili ni maalum kwa ajili ya akina mama
wenye mahitaji ya kujifungua kwa upasuaji na sasa hivi kuna vyumba 35 vya
upasuaji vikiwemo 13 maalum kwa ajili ya akina mama na vitengo vya dharura
vimeongezeka kutoka viwili hadi 13.
Awali, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed
Mussa alitumia fursa hiyo kutaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana upande wa
sekta ya elimu katika kipindi cha miaka 60 ya Mapinduzi kuwa ni pamoja
kuongezeka kwa Bajeti ya sekta ya elimu kutoka shilingi bilioni 265.5 mwaka
2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 457.2 katika mwaka 2022/2023 sawa na
ongezeko la asilimia 72.2.
Alisema kiwango hicho cha bajeti katika historia ya Zanzibar
ni kielelezo cha dhamira ya Serikali katika kuendeleza Sekta ya Elimu, ambapo
kwa sasa imejipanga kujenga shule 25 za ghorofa katika maeneo mbalimbali ya
Unguja na Pemba kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024; ikiwemo shule hiyo ya ghorofa
tatu (G+3) ya Muungano.
Alisema mafanikio mengine ni pamoja na kuongezeka kwa idadi
ya shule zinazotoa elimu ya maandalizi kutoka shule moja tu mwaka 1964 hadi
kufikia skuli 891 mwaka 2023. Aidha katika kipindi hicho shule zinazotoa elimu
ya msingi zimeongezeka kutoka 62 hadi 649, shule za Sekondari zimeongezeka
kutoka tano na kufikia shule 318 mwaka 2023.
“Uandikishaji wa wanafunzi katika ngazi zote za elimu
(Maandalizi, Msingi na Sekondari) umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka
wanafunzi 25,432 mwaka 1964 na kufikia wanafunzi 592,781 mwaka 2023. Ukuaji huu
wa uandikishaji wa wanafunzi umetokana si tu kwa sababu ya ongezeko la idadi ya
watu bali pia elimu kuwa ni haki ya msingi kwa kila mtoto.
Matokeo ya mitihani ya taifa kwa wanafunzi wetu yameimarika
kwa kiasi kikubwa kutokana na uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu. Kwa Mwaka
2023, matokeo ya mitihani ya kidato cha nne asilimia ya ufaulu imeongezeka
kutoka 55.4 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 74.0 mwaka 2022.”
Aidha, kwa upande wa ya Kidato cha Sita, matokeo ya mitihani
yanaonesha kuwa, kati ya wanafunzi 2,587 waliofanya mtihani huo wanafunzi 2,570
sawa na asilimia 99.3 wamefaulu kuendelea na masomo ya chuo kikuu katika
kiwango cha Divisheni I hadi 3. Kati yao, asilimia 65.9 wamefaulu katika masomo
ya sayansi.
Pia, Waziri Lela alisema Serikali imefanya mapitio ya
mitaala ya elimu ya maandalizi na msingi kukidhi mahitaji ya sasa ya kusoma kwa
kuzingatia umahiri Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya mapitio pia kwa mtaala wa
elimu ya Sekondari kukidhi mahitaji ya umahiri na kuimarisha elimu ya amali na
ufundi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, JANUARI 15, 2024.
0 Maoni