Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini
(TARURA) Mhandisi Victor Seff amefanya ziara ya kukagua barabara ya
Lengai-Lemkuna-Msitu wa Tembo yenye urefu wa Km. 89 wilayani Simanjiro.
Katika ziara hiyo Mhandisi Seff aliambatana na Mbunge wa
Jimbo la Simanjiro Mhe. Christopher Ole Sendeka na kujionea uharibifu wa
barabara hiyo uliosababishwa na mafuriko.
Aidha, Mhandisi Seff amemwagiza Meneja wa TARURA mkoa wa
Manyara kumwelekeza Mkandarasi
Afritrust kurudi eneo la kazi ili
kuendelea kutekeleza mkataba wake kama alivyoingia.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mhe. Christopher Ole Sendeka amesema barabara hizo ni kiungo muhimu kati ya Makao
Makuu ya Wilaya ya Simanjiro na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na pia
barabara hiyo ni ya kiuchumi na imekua ikiingizia Halmashauri hiyo mapato
makubwa kutokana na kusafirisha madini ya mchanga ambapo asilimia kubwa
hutumika na wananchi wa wilaya ya Moshi katika ujenzi wa nyumba.
Hata hivyo Mbunge huyo
alimuomba Mtendaji Mkuu kuangalia uwezekano wa TARURA kufanya ujenzi wa
barabara tatu za Msitu wa Tembo-Lemkinai-Langai Km. 25,
Nabelela-Landanai-Lemkunae pamoja na
ufunguzi wa barabara ya Msitu wa Tembo-Naisinyai Km. 20 ili kuweza
kuchochea shughuli za kijamii.
Awali Diwani wa Kata ya Msitu wa Tembo Mhe. Keliya Mollel
alieleza kwamba eneo hilo lilishakumbwa na mafuriko mengine mwaka 1998
yaliyofika hadi kwenye makazi hivyo aliomba Makalavati zaidi yaongezwe kwenye
barabara hiyo ili maji yaweze kutoka kwa urahisi
Wakati huo huo Meneja wa TARURA Wilaya ya Simanjiro Mhandisi Naftal Chaula ametaja sababu kubwa za kuchelewa kukamilika kwa mradi huo ni kutokana na mafuriko yaliyoharibu kazi zilizokuwa zikifanyika na Mkandarasi na kupelekea kufanya mapitio ya usanifu na kuonekana kuna ongezeko la Makalavati manne(4) ili kuweza kudhibiti maji katika eneo la mradi.
Utekelezaji wa mradi huo ulianza mwaka wa fedha 2023/2024 kwa bajeti kutoka Serikali kuu na utekelezaji wake umefikia asilimia 60.
0 Maoni