Waliokutwa na nyara za serikali jela miaka 100

 

Mahakama ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza imewahukumu kifungo cha miaka 100 jela, watu watano kwa makosa matano likiwemo la kukutwa na  meno saba ya tembo.

Hukumu ya kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5/2022, imetolewa jana Januari 4,2023 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya hiyo, Tumsifu Barnabas huku kila kosa likiwa na kifungo cha miaka 20.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Barnabas amewataja waliohukumiwa kifungo hicho kuwa ni Mkazi wa Ushirombo mkoani Geita, Samson Emmanuel (48), Mkazi wa Itigi mkoani Singida, Shalali Jisandu (40), Hamis Ngurumo (52), Mohammed Nasibu (32) na mkazi wa Doroto, Mathayo Robert (48).

Kinyume na kifungu namba 86(1) na (2)(c)(iii) cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori namba 283 ya mwaka 2002 ikisomwa pamoja na aya ya 14 na Kifungu namba 57(1) na 60(2) cha Sheria ya kudhibiti uhalifu wa kiuchumi namba 200 ya mwaka 2022, watu hao walikutwa na hatia ya kukutwa na meno saba ya tembo na silaha ya kivita aina ya G3.

Hakimu huyo amesema ametoa hukumu hiyo baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa Jamhuri katika shauri hilo.

"Mahakama baada ya kusikiliza ushahidi wa jamhuri katika shauri hili imejiridhisha pasi na shaka kwamba washtakiwa mna hatia na inawahukumu kwenda jela miaka 100 kila mmoja," amesema Hakimu Barnabas.

Awali, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mkaguzi wa Polisi, Nyamhanga Mayagi, akisoma makosa yao, amesema kwa maeneo tofauti Julai 16,2022, walikutwa na meno saba ya tembo mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye thamani ya Tsh 138,957,000 (USD 60,000).

Pia, walikutwa na silaha ya kivita aina ya G3 ikiwa na risasi 3 kinyume cha kifungu namba 20(1)(a)(b) na 2 cha Sheria ya udhibiti wa silaha na vilipuzi namba 2 ya mwaka 2015, aya ya 31 na kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheri ya kudhibiti uhalifu wa kiuchumi namba 200 ya mwaka 2022.

Chapisha Maoni

0 Maoni