Kaya zingine 30 zahamia Msomera kutoka Hifadhi ya Ngorongoro

 

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) Bw. Mobhare Matinyi amesema kuwa jumla ya kaya 30 zenye watu 224 na mifugo 339 kutoka kwenye eneo la hifadhi ya Ngorongoro zinahamia leo kijijini Msomera katika mwendelezo wa zoezi la uhamiaji kwa hiari.

Akiongea katika mkutano wake na waandishi wa habari leo Ijumaa tarehe 5 Januari, 2024 Jijini Dar es Salaam, Bw. Matinyi ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali amesema hili ni kundi la kwanza katika awamu ya pili la wananchi wanaohamia Msomera.

Amesema kundi hili linakwenda kuungana na wananchi wengine 3,010 kutoka kwenye kaya 551 zenye mifugo 25,521 ambao walihamia kwenye awamu ya kwanza baada ya nyumba 503 kukamilika kijijini Msomera.

Aidha, amesema  kundi jingine la kaya 25 zenye watu 172 na mifugo 213 nalo linahama kutoka Ngorongoro kwenda maeneo mengine ya nchi ambayo ni mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Siminyu na Tanga.

Hili ni kundi la tatu la wanaohamia maeneo mengine katika awamu hii ya pili, amesema Bw. Matinyi.

Ameeleza kuwa wananchi wengine waliohamia kwenye maeneo mengine ya nchi nje ya Msomera ni kaya 27 zenye watu 120 na mifugo 769. Hii inafanya jumla ya waliohamia nje ya Msomera kuwa kaya 52, watu 292 na mifugo 982.

“Hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2023, tayari nyumba 350 zimeshakamilika kijijini Msomera. Hivyo basi, zoezi la kuhama litaendelea kwa mwezi huu wote wa Januari 2024,” amesema Bw. Matinyi na kuongeza, “Tayari kuna kaya 500 zilizojiandikisha huko Ngorongoro zikiwa tayari kuhama ambapo kaya 406 kati ya hizo zimeshafanyiwa tathmini ya malipo yao ya fidia na ya ziada”.

Amesema Serikali inaendelea kusisitiza kwamba zoezi hili ni la hiari kwa sababu kuu mbili: moja, ni kuwahamishia wananchi wa Ngorongoro kwenye eneo bora na pili kwa ajili ya maendeleo yao ya huduma za kijamii pamoja na usalama wao.

Pia, ni kuendeleza na kutunza uhifadhi wa eneo la Ngorongoro ambalo linaheshimika kimataifa kama moja ya maeneo ya urithi wa dunia, amesema Matinyi.


Chapisha Maoni

0 Maoni