Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Taifa
ya Moyo ya nchini Zambia wataendelea kushirikiana katika mafunzo, kufanya
tafiti na kambi za uchunguzi na upasuaji wa moyo.
Hayo yamesemwa jana na Dkt. Agness Mtaja wakati akiongea na
waandishi wa habari kuhusu kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto
inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na wenzao wa hospitali ya Taifa ya Moyo ya Zambia.
Dkt. Agness ambaye ni Mkuu wa huduma za Afya katika
Hospitali hiyo alisema kabla ya kuanza
kwa ushirikiano huo mwaka 2022 walikwenda JKCI kujifunza na kuona huduma za matibabu ya moyo
wanazozitoa ndipo mwaka jana wakasaini makubaliano ya kushirikiana ili wananchi
wa Zambia wapate huduma za matibabu ya
moyo katika nchi zao za Afrika.
“Nchi za Zambia na Tanzania zinahistoria kwani
tunashirikiana katika mambo mbalimbali ikiwemo bomba la mafuta la TAZAMA na
usafri wa reli ya TAZARA na hivi sasa tunashirikiana kutoa huduma za upasuaji
wa moyo kwa watoto na mafunzo kwa wataalamu wetu wa afya. Ushirikiano huu ni
mzuri kwani nchi ya Afrika inaisaidia nchi nyingine ya Afrika katika kutoa
huduma za matibabu ya moyo.”
“Mwaka jana tuliwapeleka wauguzi watatu JKCI kwenda
kujifunza jinsi ya kuwahudumia wagonjwa mahututi na wa dharura ambao
wameshamaliza masomo yao na wamesharudi
nchini na katika kambi hii wanashirikiana na wenzao wa JKCI kuhudumia
watoto waliofanyiwa upasuaji”,alisema Dkt. Agness.
Dkt. Agness alisema mwaka huu watawapaleka wataalamu tisa ambao
ni madaktari wa upasuaji wa moyo, mitambo, usingizi na wagonjwa wanaohitaji
uangalizi maalumu, wauguzi na wataalamu wa kuendesha mashine ya kuusaidia moyo
na mapafu kufanya kazi kwenda kujifunza zaidi kwani Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete imeendelea zaidi katika upasuaji wa aina mbalimbali wa moyo
ukilinganisha na Hospitali hiyo yaTaifa ya Moyo ya Zambia.
“Tunaishukuru Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwatuma wataalamu hawa katika Hospitali yetu
ambao tunashirikiana kufanya upasuaji na kuokoa maisha ya watoto wenye matatizo
ya moyo,” alishukuru Dkt. Agness.
Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa
watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau alisema kambi
hiyo ya upasuaji wa moyo inakwenda sambamba na kuwajengea uwezo wataalamu wa
hospitali hiyo wa jinsi ya kufanya upasuaji pamoja na kuwahudumia wagonjwa hao.
“Tumekuja na timu ya wataalamu tisa iliyokamilika katika
upasuaji wa moyo kila mtaalamu anatoa mafunzo kwa wataalamu wenzake wa hapa hii
itasaidia hata pale tutakapoondoka wataendelea kutoa huduma iliyokamilika kwa
wagonjwa.”
“Kambi hii ilianza kwa kufanya uchunguzi kwa watoto 15 ili
kubaini ni watoto wangapi wanatakiwa kufanyiwa upasuaji baada ya uchunguzi
waligundulika watoto 10 ndiyo wanahitaji huduma ya upasuaji.”
“Leo (jana) ni siku ya pili tangu tumeanza kufanya upasuaji
na tumeshawafanyia watoto wanne ambao wanaendelea vizuri ninaamini hadi siku ya
jumapili tutakuwa tumefanya upasuaji kwa watoto saba au nane na watoto wengine
watakaobaki watafanyiwa upasuaji na wenzetu hawa wa Zambia”, alisema Dkt
Sharau.
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Hospitali
ya Taifa ya Moyo ya Zambia Mudaniso Ziwa alisema matatizo ya moyo yako ya aina
mbili kuna ya kuzaliwa nayo na mengine mgonjwa anayapata ukubwani hii ni
kutokana na mtindo mbaya wa maisha watu wanaoishi hii ikiwa ni pamoja na
kutokufanya mazoezi, kutokula vyakula bora, uvutaji wa sigara na unywaji wa
pombe uliokithiri.
“Kuna watoto wengi wanazaliwa na matatizo ya moyo ambayo ni
matundu, valvu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake. Ni
vizuri watoto hawa wakapata matibabu hapa nchini na wasiende kutibiwa nje ya
nchi labda kwa upasuaji unaohitaji utaalamu wa hali ya juu ambao sisi hatuwezi
kuufanya.”
“Ninawashukuru wataalamu wa JKCI ambao wamekuja hapa kwetu
na tunafanya nao upasuaji ninaamini ushirikiano huu utakuwa endelevu kwani
utatusaidia na sisi tuweze kufika hatua ambayo wao wamefikia na kuweza kuokoa
maisha ya watoto wetu wenye matatizo ya moyo.” alisema Dkt. Ziwa.
Nao wauguzi watatu ambao walipata mafunzo ya jinsi ya
kuwahudumia wagonjwa mahututi na dharura katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) walishukuru kwa mafunzo waliyoyapata na kusema kuwa yamewajengea uwezo
wa kuwahudumia wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo.
“Mafunzo niliyoyapata JKCI yananisaidia kuweza kuwahudumia
wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo kwani wagonjwa hawa wakiwa katika chumba
cha uangalizi maalumu (ICU) wanahitaji kupata huduma ya ziada, ninawaomba na
wauguzi wenzangu waweze kuhudhuria mafunzo haya kwani yatawasaidia katika
utendaji wao wa kazi za kila siku,” alishukuru Grivas Pharaoh.
Kufanyika kwa kambi hii ya upasuaji wa moyo ni utekelezaji
wa mkataba wa miaka mitatu wa makubaliano baina ya JKCI na Hospitali ya Taifa ya Moyo ya Zambia wa
kutibu wagonjwa, kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa Hospitali hiyo wa jinsi
ya kuwatibu wagonjwa wa moyo ambao ulisainiwa tarehe 20/04/2023 jijini Dar es
Salaam.
Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH la nchini Israel ndilo lililowezesha kusainiwa kwa mkataba huo pamoja na kufanyika kwa kambi hiyo ya upasuaji wa moyo kwa watoto nchini Zambia kwa kutoa vifaa tiba na kuwasafirisha wataalamu wa JKCI.
0 Maoni