Wito umetolewa kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za
kiafya ikiwemo kudumisha usafi wa mazingira katika maeneo yao ili kuzuia
magonjwa ya mlipuko, katika kipindi hiki ambacho mvua zimekuwa zikinyesha.
Wito huo umetolewa Jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi
Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Wizara ya Afya Dkt. Tumaini Haonga ambapo
amesema mvua zinaponyesha kuna uwezekano wa athari za afya zinazoweza
kujitokeza ikiwemo uharibifu wa miundombinu ya majitaka hali inayoweza
kusababisha kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko.
“Kutokana na Mvua zinazoendelea kunyesha,kuna athari za
kiafya zinazoweza kujitokeza ikiwemo uharibifu wa miundombinu ya majitaka
ambayo yanaweza kuchangia au kuibua kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko kama vile
ugonjwa wa Kipindupindu lakini kuongezeka kwa magonjwa yanayosababishwa na
minyoo, homa ya matumbo, kwa hiyo nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi
wenzangu na jamii kwa ujumla kwa kipindi hiki mvua zinaendelea katika maeneo
mbalimbali wazingatie kanuni za afya kwa kudumisha usafi wa mazingira na
kuepusha maji kutuama kwenye maeneo ya makazi,” amesema Dkt. Haonga.
Ikumbukwe kuwa kutokana na utabiri wa hali ya hewa uliotolewa na Mamlakaya Hali ya Hewa nchini, kuna uwezekano wa kuwepo kwa mvua juu ya wastani uwepo wa El Nino hadi Januari 2024 hasa katika mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Kigoma, Morogoro, Pwani , Dar Es Salaam, Tanga, Arusha, Manyara, na Kilimanjaro.
0 Maoni