Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi, amewataka
wananchi kupuuza upotoshaji wa taarifa unaofanywa kwenye mitandao ya kijamii na
baadhi ya watu na vyombo vya habari visivyofuata maadili ya kazi kuhusu misaada
inayotolewa kwa waathirika wa maporomoko ya tope yaliyotokea wilayani Hanang,
mkoani Manyara.
Bw. Matinyi ametoa rai hiyo leo mjini Njombe katika mkutano
wa Mkuu wa Mkoa akiwa na Wakurugenzi wa Halmashauri na Waandishi wa Habari
unaoratibiwa na Idara ya Habari (Maelezo) kwa lengo la kutangaza miradi ya
maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
“Mambo yanayoandikwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu
upotevu wa misaada ya Hanang si ya kweli; na kwamba wananchi waliopokewa katika
kambi walifikia 689 kutoka kaya 139 na kwa hiari yao wenyewe waliomba warejee
kwa ndugu zao au makwao kwa sababu wengine hawakupoteza nyumba bali
ziliharibika au ziliingia tope,” alisema Bwana Matinyi.
Aidha, amearifu kwamba Rais Samia Suluhu Hassan alisema
baada ya tathmini serikali itawajengea nyumba watu wote waliopoteza nyumba zao
katika maafa haya.
“Kila mwananchi aliye kwenye kambi anapewa uhuru wa kuamua
na akiondoka anapewa misaada stahiki ambaoo katika awamu ya kwanza kila
aliyeondoka alipewa chakula cha kutosha siku 30, vifaa na vitu binafsi na vya
ndani lakini tumekwenda awamu ya pili ambapo kila walioacha maelezo yao
wanapelekewa misaada kwenye kata wanapoishi na wanapewa vitu vinavyotosha kwa
muda wa miezi sita,” amearifu Bw. Matinyi.
Aliongeza kwamba waathirika hao wanapewa vyakula vya kutosha
miezi sita na kwa sukari ni inayotosha kwa matumizi ya miezi 19; kuna unga wa
uji wenye virutubisho kwa ajili ya watoto, majiko, sabuni, magodoro, na vitu
vingine vingi vya ndani isipokuwa samani.
Msemaji Mkuu aliongeza zaidi kuwa hata wale ambao
hawakuhamia kambini nao wamesaidiwa chakula na vitu muhimu na kwamba misaada ya
chakula na vitu imefikia shilingi bilioni mbili.
Alisema pia fedha zilizokusanywa hadi kufikia tarehe 20 Desemba, 2023, ni shilingi bilioni 5.2 akieleza fedha hizo zimeingizwa kwenye akaunti moja ya maafa inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Na. Mwandishi Wetu- Njombe
0 Maoni