WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la
Ruangwa jana (Alhamisi, Desemba 21, 2023) amefanya ziara kwenye vijiji vinne vya
kata ya Mbekenyera, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Vijiji alivyovitembelea na kuzungumza na wakazi wake ni
Chingumbwa, Mkutingome, Naunambe na Mbekenyera.
Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Chingumbwa katika kata
ya Mbekenyera, Mheshimiwa Majaliwa amesema katika kipindi cha miaka miwili,
kata hiyo imepatiwa sh. bilioni 2.5 za utekelezaji wa miradi ya maendeleo
ikiwemo ya sekta za afya na elimu.
Pia amewataka wakazi hao waendelee kuwa na imani na Serikali
ya awamu ya sita kwani imedhamiria kutatua kero zao. “Mheshimiwa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan ana dhamira ya dhati ya kushirikiana na wana-Ruangwa na
Watanzania wote katika kutatua changamoto zilizopo hivyo endeleeni kuwa na
imani naye, na muwe na imani na Serikali yenu ya awamu ya sita,” amesema.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia kikamilifu ujenzi
na ubora kwenye sekta ya elimu kuanzia shule ya msingi ili watoto wasitembee
umbali mrefu kufuata shule.
Akiwa kwenye kijiji cha Mkutingome, Waziri Mkuu ameagiza
RUWASA wilaya ya Ruangwa ikamilishe kwa wakati mradi wa maji utakaohusisha vijiji
vya Chingumbwa na Mkutingome ili wananchi hao waanze kupata huduma ya maji safi
na salama.
Ili kuharakisha kukalimika kwa mradi huo, Waziri Mkuu
amesema: “Natambua kuwa ujenzi huo utahusisha uwekaji wa vilula, kazi hii
msiitoe kwa mkandarasi mmoja, gaweni kazi, mmoja apewe chanzo tu, mwingine njia
za maji na mwingine ajenge vilula,” amesema.
Akitoa maelezo kuhusu mradi huo, Kaimu Meneja wa RUWASA,
wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Rashid Shabani amesema kuwa wanaendelea na taratibu
za ujenzi wa mradi huo ambao unategemea kuzalisha zaidi ya lita 5,000 kwa saa.
“Mpaka sasa tumeshafanya tafiti na kuchimba kisima na
tunaendelea na kuangalia ubora wa maji, yote haya tutayafanya katika mwaka huu
wa fedha,” amesema.
Akiwa kijiji cha Naunambe, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa
shule mpya ya sekondari ya Nambawala na kusema ameridhishwa na ubora wa viwango
vya ujenzi wa shule hiyo. Amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma
aendelee kuwatumia wakandarasi hao.
Katibu wa mradi huo, Hussein Juma Omari alisema Juni 30,
mwaka huu, Kata ya Mbekenyera, ilipokea sh. milioni 560.5 kutoka Serikali kuu
kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya chini ya Programu ya Uboreshaji wa Elimu ya
Sekondari (SEQUIP) ambapo hadi sasa zimetumika sh. milioni 510. Ujenzi huo
unatarajiwa kukamilika Desemba 30, 2023.
Akiwa kijiji cha Mbekenyera, Waziri Mkuu alitembelea kituo
cha afya na kukagua utoaji wa huduma kwenye kituo hicho. Alimwagiza Kaimu
Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt. Boniface Nonga afuatilie matengenezo ya gari
la wagonjwa ili liweze kuwahudumia wananchi wa vitongoji vya jirani.
Akizungumza na wakazi wa kijiji hicho, aliwasisitiza vijana wa kata hiyo watumie fursa ya uwepo wa madini ili kukuza uchumi wao na waende Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) ili wapate ujuzi na kuboresha stadi kwenye uchimbaji wa madini.
“Vijana, akinamama, na wazee wenzangu, tuna fursa ya madini ya graphite (bunyu), tujipange kuanza kunufaika na fursa hii, vijana nendeni mkaongeze ujuzi VETA, fungueni maduka, jengeni nyumba za wageni, kwani madini ni uchumi.”
0 Maoni