Serikali inaendelea na utekelezaji wa shughuli za usafi wa mazingira na uboreshaji wa miundombinu ya matundu 100 ya vyoo katika shule zilizokuwa zikitumika kuhifadhi waathirika wa maporomoko ya udongo wilayani Hanang Mkoani Manyara.
Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa afua mbalimbali zenye
lengo la kurudisha hali katika uhalisia wake. Uboreshaji wa vyoo katika Shule
hizi unasaidia kuweka utayari wa mazingira safi pindi shule zitakapofunguliwa
Mwezi Januari.
Mkuu wa Sehemu ndogo ya Maji na Usafi wa Mazingira kutoka
Wizara ya Afya Anyitike Mwakitalima akizungumza katika zoezi la ukarabati wa
matundu 32 ya vyoo shule ya Msingi Gendabi amesema uwekaji wa matundu ya vyoo ya kisasa utasaidia wanafunzi
kufurahia Mazingira ya kujifunzia kutokana na ubora wa vyoo hivi ambavyo
hutumia maji kidogo na hudhibiti harufu
mbaya pamoja na wadudu.
“Vyoo vilivyokuwepo vilikuwa na mapungufu kadhaa ambayo
tumebaini hivyo, tumeamua kuboresha ambapo kutakuwa na faida nyingi ikiwemo
utumiaji wa maji kidogo, hakutakuwa na harufu mbaya, wadudu kama mende
hawatakuwepo na hofu ya kutumbukia haipo hata mtoto anayetambaa hawezi
kutumbukia, pia wadudu hatarishi kama nyoka hata akitumbukia hataweza kutoka
tena maana kina mfuniko unaojifunika,” amesema Mwakitalima.
Aidha , Mwakitalima
amewahakikishia Wazazi kuwa baada
ya kambi kufungwa Mazingira ya shule ni salama kwani tayari wameshanyunyizia
dawa kuondoa wadudu na mazingira
yanakuwa bora zaidi kuliko awali.
Naye Muuguzi Mkuu wa Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara Editha Jonathan amesema usafi wa mazingira na
ukarabati wa miundombinu ya vyoo utasaidia kuepuka magonjwa ya mlipuko huku
akisema usambazaji wa jumbe za uelimishaji kuhusu masuala ya afya umekuwa
ukiendelea.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkuu wa Shule ya Msingi
Gendabi Mwalimu Kindoli Twaha ameshukuru hatua hiyo ya uboreshaji wa
miundombinu ya matundu ya vyoo.
“Maboresho haya tunayafurahia sisi kama walimu maana mwanafunzi hawezi kuona tundu la choo na vinatumia maji kidogo sana,”amesema Mwalimu Twaha.
0 Maoni