Taarifa ya Serikali kuhusiana na maendeleo na hali baada ya
kutokea maafa wilayani Hanang mkoani Manyara imeeleza kuwa hadi kufikia sasa
miili iliyopatikana ni 85 na yote imeshatambuliwa na ndugu zao na kuchukuliwa.
Taarifa hiyo iliyotolewa leo wilayani Hanang na Msemaji Mkuu
wa Serikali Mobhare Matinyi imesema idadi hiyo ya vifo ipo katika mchanganuo ambao
watu wazima ni 49 (wanaume 20 na wanawake 29), na watoto 36 (kiume 16 na kike
20).
Taarifa hiyo imeongeza kwamba hadi sasa jumla ya majeruhi na
wagonjwa waliopokelewa tangu maafa ya maporomoko ya matope kutoka MlimaHanang
yatokee ni 139 lakini waliopo hospitalini ni 51.
Aidha, taarifa hiyo imesema kutokana na juhudi za Serikali
za kuwapa ushauri nasaha, kuwasaidia kupata mahitaji muhimu na chakula pamoja
na kuwaunganisha na ndugu na jamaa zao, waathirika kwenye kambi wamepungua
kutoka 440 hadi 322.
Serikali inaendelea kuwashukuru na kuwapongeza Watanzania
pamoja na taasisi za umma na binafsi za ndani ya nchi yetu kwa moyo wa utu na
uzalendo. Serikali inatoa wito kwa wanaojitolea kufanya hivyo kwa kuleta vifaa
vya ujenzi ili visaidie kuwapatia makazi mapya waathirika wa maafa haya,
imesema taarifa hiyo.
0 Maoni