Tumieni mitandao ya kijamii vizuri- Dkt. Mpango

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amewataka Watanzania kutumia mitandao vizuri na kuacha kuzusha na kusambaza habari ambazo hazina ukweli kwakuwa zinaumiza Familia za wanaozushiwa ambapo ametolea mfano kuwa mwaka 2021 alipozushiwa kifo, Dada yake (Ambaye amefariki kwa sasa) alianguka kwa mshtuko.

"Mhe. Rais nina afya njema tayari kuendelea na kazi ukiacha hizo maalum ambazo nilikuwa nashughulika nazo (Nje ya Nchi), nawashukuru sana Viongozi wote na Watanzania ambao baada ya kupata taarifa ambazo hazikuwa sahihi walipata taharuki kubwa, wengi wameniombea sana ninawashukuru kwa moyo wangu wote na hao wachache ambao wanasema maneno mengine basi nawaombea msamaha kwa Mungu”

"Natumia nafasi hii kuwaomba Watanzania wenzangu mitandao ni chombo kizuri lakini matumizi yake nawaomba tutumie mitandao vizuri, unajua ukisema huyu Mzee amekata moto wengine wanaweka picha yangu na mshumaa unawaka lakini Mh. Rais sisi Viongozi ni Binadamu tuna Watoto tuna Wajukuu, tuna Familia , tuna Marafiki na Wafanyakazi wenzangu, taharuki kubwa sana ambayo haina sababu”

“Mwaka 2021 Dada yangu ambaye nilimzika mwezi wa nane, alipoambiwa kwamba Mimi Mwanae kwasababu alinilea nimefariki alianguka akiwa Mama wa miaka 80, sio mambo mema ni vizuri tutumie mitandao kwa mema kuwatakia kheri Watanzania wenzetu"

"Mhe. Rais uliponiapisha nilisema unitume mchana na usiku, ulinituma huko (Nje ya Nchi) nimerejea nchini tayari Kuendelea na kazi”

Hayo yamesmwa na Mjumbe wa  Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza mara baada ya kukutana na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ,Ikulu Chamwino Jijini Dodoma, leo tarehe 10 Desemba, 2023.

Chapisha Maoni

0 Maoni