Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb)
amesema Tamasha la Kilimanjaro Cultural Festival linalohusisha utamaduni wa
vyakula ,ngoma na lugha za asili za jamii ya Wachaga, Wapare na Wamaasai
litasaidia kukuza utalii wa Mkoani Kilimanjaro endapo litaendelezwa na kutumika
ipasavyo.
Amesema lengo la Tamasha hilo ni kukuza na kuhamasisha
utalii wa malikale ndani ya Mkoa wa
Kilimanjaro sambamba na kuenzi mila na desturi za jamii za Mkoa huo zinazojumuisha Wapare,
Wachaga na Wamaasai.
Ameyasema hayo leo Desemba 28, 2023 alipokuwa akifunga
tamasha hilo lililofanyika katika viwanja vya Kili Home Garden, Moshi Mjini
Mkoani Kilimanjaro.
“Nimeshuhudia vyakula vya kiasili vya jamii za Mkoa wa
Kilimanjaro vilivyoandaliwa kwa ustadi mkubwa,
tukio hili limenikumbusha masuala ya afya kuhusu umuhimu wa vyakula vya
asili ikiwa ni pamoja na kukinga miili
yetu na kujenga nguvu mwilini na hii
ndiyo sababu zamani Wazee wetu waliishi miaka mingi bila ya kusumbuliwa na
maradhi ya mara kwa mara.” Mhe. Kairuki
amesisitiza.
Pia, amesema ameshuhudia ngoma za asili za kipare, kimaasai
na kichaga, lugha za asili za Kipare, Kimaasai na Kichaga ambazo zinawakumbusha
vijana kuenzi mila na tamaduni zao ili waweze kufahamu walikotoka na
wanakoelekea.
“Natoa wito kwa vikundi vya ngoma kuendelea kukutana kila
wakati na kubadilishana uzoefu baina ya kikundi kimoja na kingine kwa sababu
ngoma za asili ni kivutio kikubwa kwa watalii wanaokuja kutembelea vivutio
vyetu nchini Tanzania” Mhe. Kairuki amesema.
Katika hatua nyingine Waziri Kairuki amezindua program ya
‘’Kilimanjaro Home Stay’’ inayohusu utaratibu wa kutumia nyumba za wenyeji
kutoa huduma za malazi kwa wageni hususan kipindi cha matukio makubwa kama vile
mbio za Kilimanjaro Marathoni ili kukuza vipato kwa jamii moja kwa moja.
Ameipongeza Taasisi ya Kilimanjaro Cultural Festival kwa
kuunga mkono jitihada za Serikali za kufanya utafiti na kuhifadhi nyaraka na
kumbukumbu za Urithi wa Utamaduni usioshikika wa jamii ya Kilimanjaro ikiwa ni
pamoja na kuandaa kanzidata ya maeneo ya malikale yaliyopo ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Naye,Mwenyekiti wa Kilimanjaro Cultural Festival, Hans Mmasi amesema tamasha hilo linaunga
mkono juhudi za Serikali za kutangaza utalii nchini na linalenga kuwakutanisha
wadau mbalimbali wa maendeleo katika sekta ya utalii, utamaduni na biashara.
Ameongeza kuwa tamasha hilo lina matarajio ya kuvutia wageni
na watalii wapatao elfu kumi ifikapo
mwaka 2028.
Tamasha hilo limeratibiwa na
Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Kilimanjaro Cultural Festival ambayo
ilitokana na Jukwaa au Group la Whatsapp lijulikanalo kama ‘’Kilimanjaro
Maendeleo Group’’, ambalo kwa sasa lina wanachama wapatao 400.
Tamasha hilo limehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiongozi wa Machifu wa Jamii za Mkoa wa Kilimanjaro, Mangi Frank Mareale, Viongozi wa Dini, Viongozi Mbalimbali wa Vyama vya Siasa na Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Na Happiness Shayo
0 Maoni