Mitaala mipya ya mafunzo ya uhandisi maji kuanza mwakani

Serikali inaendelea kukamilisha mchakato wa kukukusanya na kupitia maoni ya mitaala mipya itakayotumika kutoa mafunzo ya programu ya uhandisi maji na maendeleo ya jamii ilikuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na kukidhi mahitaji ya soko la ajira.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akiwa kwenye warsha ya mapitio ya mitaala ya programu ya uhandisi maji na maendelo ya jamii iliyowakutanisha wahandisi maji, ujenzi na maendeleo ya jamii iliyofanyika katika chuo cha maendelo ya jamii ufundi Misungwi mkoani Mwanza amesema wanatarajia mitaala mipya itaendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Mpanju amesema mitaala hiyo mipya itasaidia vijana wanaojiunga na vyuo kupata mafunzo yanayoendana na mahitaji na mazingira ya sasa na kuwashukuru NACTVET kwa namna walivyotoa miongozo mbalimbali ya kuboresha mafunzo hayo.

“Kazi kubwa hasa tuliyonayo hapa ni kuboresha maeneo yote ya msingi ya mitaala yaani kuaniza maudhui hadi upimaji na tathmini yatakayojumuishwa katika ngazi mbalimbali za mafunzo, maoni mtakayotoa yataingizwa kwenye mitaala inayofanyiwa kazi mapitio kwa kuzingatia mahitaji ya soko la ajira,” amesema Mpanju.

“Naiagiza Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na vyuo kuhakikisha kuwa inafanyia kazi maoni yote yatakayotolewa na wadau ili mitaala hii iweze kuakisi uhalisia wa mahitaji ya soko la ajira”.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo Taaluma cha Maendeleo ya Jamii Ufundi Misungwi Mwanza, Dongo Nzori amesema lengo la kuanzishwa kwa mitaala hiyo mipya ni kupunguza changamoto zilizopo kati ya wahandisi uwiano kati ya wahandisi na mafundi sanifu na mchundo hiyo ni kutokana na hitaji la soko la ajira la sasa

“Sisi tunazalisha wahandisi sana lakini wanafanya kazi za usimamizi wa miradi lakini nani anakaa kule kwenye miradi ndiyo tunahitaji wataalamu ndiyo uanzishwaji wa hivi vyuo vyetu,” amesema Nzori.

Akiwa kwenye warsha hiyo Mhandisi Wibert Bujiku kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza, kanda ya Misungwi amesema sasa hivi wapo kwenye hatua ya mwisho ya kukamilisha mtaala ili hatimaye hapo mwakani mitaala hiyo ianze katika vyuo vya maendelo ya jamii ufundi Misungwi na Mabughai cha Tanga.

Mitaala ya programu ya uhandisi maji na maendelo ya jamii kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa ngazi ya astashahada na stashahada inakusudiwa kuanza kutolewa kuanzia mwakani katika vyuo vya maendeleo ya jamii ufundi Misungwi mkoani Mwanza na Mabughai Tanga.

Chapisha Maoni

0 Maoni